2015-05-12 06:59:00

Acheni mchezo, kama mambo ni hivi! Nitaanza kusali na kurudi Kanisani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 10 Mei 2015 alikutana na kuzungumza kwa faragha na Rais Raul Modesto Castro Ruz wa Cuba; mazungumzo ambayo yamefanyika katika hali ya kirafiki na kudumu kwa takribani muda wa saa nzima. Rais Raul akizungumza na waandishi wa habari anasema kwamba, hii ni ziara ya pekee katika maisha yake, ambayo imemgusa na kuitikisa sakafu ya maisha yake. Alipowasili mjini Vatican, Rais Raul alipokelewa na viongozi wakuu wa Vatican na baadaye wakawa na mazungumzo ya faragha na Baba Mtakatifu Francisko.

Rais Raul akizungumza na waandishi wa habari anasema, amekuja mjini Vatican kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa mchango wake mkubwa, uliowezesha kuanza kwa mchakato wa maboresho ya kidiplomasia kati ya Cuba na Marekani. Anasema, wananchi wa Cuba wanamsubiri Baba Mtakatifu Francisko kwa hamu kubwa atakapowatembelea mwezi Septemba 2015, akiwa njiani kuelekea Marekani.

Baba Mtakatifu alipata pia fursa ya kukutana na kuzungumza kwa ufupi na Msafara wa Rais Raul pamoja na kubadilishana zawadi. Zawadi kutoka Cuba ni kutaka kutambua mchango wa Baba Mtakatifu Francisko kama sauti ya Kinabii na Mtetezi wa wanyonge; hususan wakimbizi na wahamiaji; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu amemzawadia Rais Raul waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium pamoja na medali ya Mtakatifu Martino wa Tour anayemfunika maskini kwa joho lake, dhamana kwa viongozi kuwalinda na kuwatetea watu wao sanjari na kutetea utu na heshima yao kama binadamu.

Rais Raul pia lipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi. Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Raul kwa mara nyingine tena amekiri kwamba, ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na unyenyekevu, hekima na fadhila ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia Baba Mtakatifu Francisko. Anasema, anasoma mara kwa mara hotuba zake na kama ataendelea hivi, muda si mrefu hata yeye ataanza tena kusali na kurejea tena kwenye Kanisa Katoliki. Rais Raul anasema huu si mzaha! Yuko makini na yale anayoyazungumza.

Kwa upande wake, Matteo Renzi amezungumzia kuhusu mahusiano kati ya Cuba na Marekani na kwamba, kuna mambo mengi ambayo kwa sasa yanaendelea kubadilika kwa kasi ya ajabu. Huu ni mchango wa diplomasia ya Vatican, inayofanyka utume wake kwa uhakika, kwa subira na matumaini makuu na matokeo yake, yanaanza kuonekana. Kanisa  Katoliki nchini Cuba nalo pia linaendelea kuchangia katika mchakato wa mabadiliko nchini Cuba, Waswahili wanasema, eti mambo mazuri hayataki haraka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.