Jumapili wakati wa sala ya malaika wa Bwana , Papa akisalimia mahujaji na wageni waliokusanyika katika uwanja wa kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alitafakari somo la Injili ya Yohana, Sura ya 15, ambamo Yesu anatoa amri mpya kwa wanafunzi wake , wapendane kama yeye alivyowapenda , “Pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi".
Baba Mtakatifu alisema, maneno hayo ya Yesu, yanatoa ujumbe mzima wa maisha ya Yesu hapa duniani kwamba, Mungu alimpenda binadamu hata akamtoa mwanae pekee sadaka, ili binadamu apate tena stahili ya kuitwa Mwana wa Mungu. Ni kuwa na upendo wa sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Yesu alisema "Hakuna aliye na upendo mkuu kuliko huu: kuyatoa maisha yake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. Yesu aliwaambia wanafunzi wake wakati wa Karamu ya mwisho, katika Chumba cha juu. Huo ni muhtasari wa yote yaliyofanywa na Yesu, kuutota sadaka uhai wake kwa ajili ya rafiki zake, tena marafiki ambao walikuwa bado hawajaelewa kina cha upendo wake, wa kuwa tayari kutelekezwa, kusalitiwa na kukataliwa. Hili linatuambia sisi pia kwamba, Yesu anatupenda, hata kama hatustahili upendo wake. Yesu alitupenda hivyo!
Baba Mtakatifu aliendelea kusema , kwa njia hii, Yesu anatuonyesha njia ya kufuata, njia ya upendo. Na kwamba, amri yake si amri nyepesi , inayoweza kuchukuliwa kama kitu cha ziada au kuwa nje ya heshima na maisha. Lakini daima ni amri msingi ya kufuatwa katika maisha. Na ni amri mpya ya Kristo, kwa kuwa Kristo alikuwa wa kwanza kuifanikisha , kuutoa mwili na uhai wake kwa sababu ya binadamu mwingine na mara kuandikwa katika moyo wa mwanadamu (taz Yer 31:33), tena kwa moto wa Roho Mtakatifu.
Kwa maelezo hayo, Papa alitoa wito kwa waamini wote, kutembea katika njia hii ya upendo, akisema , ni njia halisi, inayowataka waamini kuupeleka upendo huu kwa wengine. Ni kupeleka upendo wa Mungu kwa jirani. Ni wote kutembea pamoja. Na kwa namna gani tunaweza kuwa na uhakika tunatembea katika njia kamili ya upendo huu, Papa Francisko ametoa mfano ni katika kuwajali watoto na watu wazima, wenye elimu na wasiokuwa na elimu, matajiri na maskini, watu wema na wenye dhambi, wote ni kuwakaribisha katika moyo wa Kristo. Wote ni kujazwa na upendo wa kukomboa, ni kuwekwa huru kutoka ubinafsi.
Papa aliendelea kusema, Upendo huu huchota nguvu zake kutoka Ubatizo. Na kwa neema ya Mungu na imani ya Kanisa, mbatizwa hupadikizwa katika shina la mzabibu wa kweli, ambaye ndiye Kristo. Ni kupita kutoka katika kifo hadi maisha, na kuwezeshwa kurejea kwa Mungu kama Baba . Papa anasema kuna mambo mengi madogo na makubwa ya kutenda katika kutii amri ya Bwana: "Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi". Papa ametaja kati ya ishara ndogondogo katika maisha ya kila siku ni huduma kwa wazee, watoto, mgonjwa, mtu mpweke na mwenye mashaka, watu wasio na makazi, ajira, wahamiaji, wakimbizi ... Papa alieleza na kutoa shukurani za dhati kwa nguvu ya Neno la Kristo, ambalo humwezesha kila anayeliamini , kujenga moyo wa upendo na fadhila, kwa wake kwa waume upendo wanaokubali mafundisho ya Kristo.
Baada ya hotuba yake, Papa alisalimia makundi mbalimbali, na kwa namna ya pekee alitoa salaam zake kwa kundi kubwa la watu walioshiriki katika Matembezi kwa ajili ya Maisha. Alisema ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kutetea na Kukuza Maisha. Miongoni wa kundi hilo, alikuwa ni Kardinali Raymond Burke. Pia Papa alitoa salaam zake kwa adhimisho la Siku ya Mama Dunian. Papa aliwatakia Mama wote , tunaoishi nao na hata wale wanaoishi nasi kiroho, Baraka za Bwana na kuwaweka chini ya usimamizi wa Mama Maria, Mama wa Yesu. Na kuwaomba wote wasisahau kumwombea.
All the contents on this site are copyrighted ©. |