2015-05-11 09:57:00

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu: Dunia inahitaji huruma!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo! Kwa mara nyingine tena karibu katika mwendelezo wa vipindi vya uchambuzi kutoka katika hazina ya imani yetu. Kukumbusha tu mpendwa msikilizaji, kwa wakati huu tunaichambua barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko, ijulikanayo kwa jina la Misericordiae vultus, yaani uso wa huruma, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Jubilei hiyo, itazinduliwa rasmi hapo tarehe 08 Desemba 2015, na kuhitimishwa rasmi katika Sherehe ya Kristo Mfalme, tarehe 20 Novemba 2016.

Baba Mtakatifu anatutafakarisha juu ya thamani ya huruma ya Mungu. Kwa wakati wetu huu, familia ya mwanadamu inahitaji zaidi na zaidi huruma ya Mungu kuliko wakati mwingine wowote. Ni mwaliko wa kumrudia mwenyezi Mungu mwenye huruma kwa wakati wote. Ni mwaliko pia wa kujipatanisha kwa namna ya pekee na nafsi zetu, na kwa njia hiyo tutaonja furaha na msukumo kutoka ndani mwetu wa kutamani na kupenda kujipatanishana wenzetu.

Tuitazame hali halisi ya familia ya mwanadamu leo! Ni familia iliyofitanika. Ni familia iliyojishetanisha. Na watu hawaoni aibu wala woga wa kushetanishana. Hila na tabia za kishetanishetani zinaonekana kuwa ndio u-kawaida wa maisha. Yule anayejitahidi kuendenda katika haki, katika uwepo wa Mungu, huyo ndiyo anaonekana hafai na anaharibu jamii. Ni hali halisi!

Upendo umefifia mioyoni mwa watu. Magomvi hayakomi kuanzia katika ngazi ya familia hadi jumuia ya kimataifa. Milindimo ya vita inasikika kila huko! Ulimwengu wetu umedamishwa, kwa  damu za watu zinazomwangwa kila siku kutokana na mauaji ya kinyama na kigaidi, yanayofanywa sirini au hadharani na vikundi vya watu wenye misimamo mikali ya kiimani, misimamo isiyojua utu, misimamo inayokejeli jina la Mungu. Ni hali halisi!

Tamaa ya mali na vyeo inazidi kupamba moto, hadi watawala wengine hawaoni aibu kuchezacheza na katiba za nchi zao, kujihalalishia madaraka huku wakiweka rehani amani na usalama wa raia zao. Siasa chafu za uwongo, za wizi na itikadi za kibaguzi; uwe ni ubaguzi wa rangi, wa kikabila, kidini, au ubaguzi wa kitaifa, vinazidi kushamiri sehemu mbalimbali za dunia. Watu wanapigwa na kuuawa, kwa sababu tu sio raia wa nchi fulani. Watu wanachinjwa kikatiri kwa sababu tu siyo wa dini fulani. Inasikitisha sana, lakini ni hali halisi!

Imani kwa Mungu mmoja na wa kweli imepungua. Watu tumempa Mungu kisogo huku ibada kwa mashetani zinasikika kila kona; na vikundi vya kishetani shetani vinaendelea kujiimarisha huku vikijipatia wafuasi wengi, wa siri na wa hadhara. Ugumu na usugu wa mioyo unazidi, uadilifu umepungua katika kona zote za maisha. Kanisa linazidi kushambuliwa kutoka ndani na nje. Mwanadamu leo amejaa wasiwasi mtupu. Wasiwasi, mashaka, hofu, woga, vimekuwa ndio mwendo mdundo wa maisha ya watu waliowengi. Ni hali halisi!

Tunapoyatazama yote hayo, tunajawa na maswali mengi. Kuna nini kinapita duniani nyakati zetu hizi? Kwa nini yatokee hayo yote? Je, ni utimilifu wa maandiko kama tusomavyo katika 2Tim:3:1-9, ambapo tunasoma juu ya tabia za watu katika siku za mwisho ? Au kama tusomavyo katika  Injili ya Mathayo 24:3-14, ambapo tunaelezwa  juu ya Ishara za mwisho wa nyakati? Siku ile Yesu alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake baada ya kuyasikia mafundisho yake juu ya siku za mwisho, wanamuuliza sasa wakisema “Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? 

Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.  Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu.

Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.  Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. (Mt. 24:3-14).

Baba mtakatifu anapoona na kutafakari juu ya hayo yote, anasali kuuombea ulimwengu huu, amani, mapatano ya kweli na usitawi. Anafanya bidii ya akili, mwili na roho, kuyafumbua macho na mioyo ya watu ili kuweza kutoka na kuwafikia binadamu hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anafumbua masikio ya Jumuiya ya kimataifa ili kuweza kusikia vilio vya watu vinavyoendelea kutamadunishwa kila leo sehemu mbalimbali za dunia.

Na katika roho ya sala na mwanga wa Roho Mtakatifu, Baba Mtakatifu Fransisko ndani ya Misericordiae vultus yaani Uso wa huruma,  anatualika sote kuitafakari, kuishukuru na kuomba huruma ya Mungu. Ni huruma ya Mungu tu ndiyo itakayotuokoa katika hali hii. Ni huruma ya Mungu ndiyo itakayoturudishia hadhi na heshima yetu kama waana huru wa Mungu. Ni huruma ya Mungu tu, ndiyo itakayotuondoa katika hofu, woga na mashaka tunayokuwa nayo kwa sasa. Ni huruma ya Mungu tu, ndiyo inatakayotuumbia mioyo safi na kutengeneza tena roho zilizotulia ndani mwetu (Zab. 51:10). Na hapo hapo, sisi wenyewe tunaalikwa sana kuwashirikisha wenzetu huruma hiyo ya  Mungu, inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma na upendo.

Asante kwa kuitegea sikio Radio Vatikan. Usisahau kutumia ile dawa iponyayo akili, mwili na roho ambayo Baba Mtakatifu ametusisitiza tuitumie ili tupone, yaani kusali kwa imani rozali ya huruma ya Mungu, ili atuhurumie sisi na dunia nzima.

Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.