2015-05-11 10:53:00

Msikumbatie utamaduni wa kifo, ndoa za watu wa jinsia moja na rushwa!


Hakuna sababu ya kuendelea kukumbatia utamaduni wa kifo, Serikali haina budi kuhakikisha kwamba, inatekeleza wajibu na dhamana yake kadiri ya Katiba ya Nchi; Ufisadi na rushwa havina nafasi tena nchini Kenya; ndoa za watu wa jinsia moja nchini Kenya ni kinyume kabisa cha maadili na utamaduni wa kiafrika. Serikali ina dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Haya ni mambo msingi ambayo yamejadiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni Jijini Nairobi.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limepembua kwa kina na mapana matukio ya mauaji ya watu wasiokuwa na  hatia, yanayoendelea kuitikisa nchi hadi wakati huu. Maaskofu wanawakumbuka wananchi wa Kenya waliouwawa kikatiliki kwenye shambulizi la kigaidi lililofanyika huko kwenye Chuo Kikuu cha Garissa na kusababisha watu 148 kupoteza maisha yao. Mauaji ya kinyama na ambayo kwa wakti mwingine yanafanyika kwa misingi ya kidini ni jambo ambalo kamwe, haliwezi kukubalika.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kusema kwamba, utamaduni wa kifo unaendelea kuwaandamana wananchi wa Kenya na kwamba, Serikali inapaswa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinarejeshwa tena nchini Kenya na kwamba, hii ni changamoto inayopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Uvumbuzi wa uwepo wa mafuta Kaskazini mwa Kenya, kisiwe ni kisingizio cha uvunjaji wa sheria na kwamba, Serikali inapaswa kuendesha nchi kwa kuzingatia Katiba, Serikali inayoshindwa kuwalinda raia wake, hiyo inakosa pia dhamana ya kuongoza nchi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, kamwe haliwezi kuendelea kuangalia wananchi wakipoteza maisha kutokana na vitendo vya kigaidi. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, silaha ambazo zimezagaa sana miongoni mwa wananchi zinadhibitiwa sanjari na kuanzisha sera na mikakati ya kiuchumi na kijamii, itakayowajengea wananchi uwezo kiuchumi pamoja. Mikakati hii haina budi kwenda sanjari na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na wale wote wanaotuhumiwa wasimamishwe kazi mara moja na uchunguzi wa haraka, makini na unaozingatia haki ufanyike. Wananchi wote wa Kenya wanapaswa kushikamana ili kuhakikisha kwamba, rushwa na ufisadi vinakomeshwa na hatimaye kutoweka kabisa nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitishwa sana na maamuzi yaliyotolewa hivi karibuni na Mahakama kuu ya Kenya ya kuruhusu watu wa jinsia moja kufunga ndoa; dhana ambayo inakwenda kinyume kabisa cha utu wema, maadili, mila na tamaduni njema za Kiafrika; uamuzi huu unatishia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, ni uamuzi unaokwenda kinyume cha Katiba ya nchi. Maaskofu wanaitaka Serikali kuwa makini zaidi na kamwe isiruhusu Kenya kuwa ni uwanja wa majaribio kwa Sera za kigeni. Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Kenya, kusali kwa ajili ya kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Maaskofu wanabainisha kwamba, wao wataendelea kuikumbusha Serikali umuhimu wa kuzingatia Katiba ya nchi, kulinda Uhai pmoja na kutoa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.