2015-05-09 17:55:00

Sinodi ya Jimbo kuu la Tabora: sifa za Kanisa mahalia!


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kuungana na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora, Tanzania katika kusherehekea na kumpongeza Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anapoadhimisha kilele cha Jubilee ya miaka 25 tangu alipowekwa wakfu. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia.

Itakumbukwa kwamba, Jimbo kuu la Tabora hivi karibuni limehitimisha maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Yesu hu seba”, Yesu ni taa ya uhai wa imani ya watu wake. Jimbo kuu la Tabora, tayari limekwisha chapisha maamuzi ya Sinodi ambayo kwa sasa yanapasw akumwilishwa katika maisha na vipaumbele vya Jimbo kuu la Tabora.

Askofu mkuu Ruzoka anasema, Kanisa mahalia kadiri ya mang’amuzi ya Mababa wa Sinodi ya Jimbo kuu la Tabora, linapaswa kujipambanua kwa kuwa na Kiongozi wake mkuu, anayesaidiwa na Mapadre, Watawa, Makatekista na Baraza la Halmashauri Walei. Sifa ya pili ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linajenga na kudumisha mwelekeo wa kimissionari, kwani linatumwa kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, ushuhuda unaojikita katika utakatifu wa maisha.

Askofu mkuu Ruzoka anasema kwamba, Kanisa mahalia halina budi kuwa na uhakika wa vyanzo vya mapato yake, ili kutekeleza kwa dhati mikakati ya shughuli za Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Kanisa mahalia halina budi kujiwekea mikakati ya kujitegemea kwa kuhakikisha kwamba, waamini wanachangia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa. Mali ya Kanisa halina budi kusimamiwa na kuratibiwa vyema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.