2015-05-09 17:11:00

Simameni kidete kuwalinda na kuwatetea watoto dhidi ya nyanyaso!


Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya watoto ndani ya Kanisa na kwamba kusiwepo tena matukio ya nyanyaso dhidi ya watoto ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anayasema haya katika Katiba ya Tume ya Kipapa ya kuwalinda watoto, iliyoanzishwa tarehe 22 Machi 2014. Katiba hii ambayo kwa sasa imeanza kutumika kwa majaribio katika kipindi cha miaka mitatu, imeidhinishwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa idhini ya Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linajitahidi kufanya kila kinachowezekana, ili kutokomeza nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo yaliyojitokeza katika baadhi ya maeneo ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka wasaidizi wake wa karibu kumpatia ushirikiano wa kutosha ili kuweza kutekeleza mahitaji msingi ya ulinzi na usalama kwa watoto wadogo.

Lengo ni kuendeleza dhamana iliyokuwa imeanzishwa na watangulizi wake ili kuhakikisha kwamba, Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa na Makanisa mahalia wanasaidia mchakato wa kuwalinda watoto na watu wazima ambao wanaweza kuwa ni wahanga wa nyanyaso za kijinsia. Tume hii ya Kipapa itashirikiana na watu binafsi au makundi ya watu ili kutekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakumbuka machungu na adha iliyosababishwa na nyanyaso na dhuluma dhidi ya watoto wadogo, jambo ambalo linalitaka Kanisa kuchunguza dhamiri yake kwa umakini mkubwa, ili kuomba msamaha kwa waathirika na jamii katika ujumla wake, kutokana na madhara haya; kutoa fidia na kutenda haki pamoja na kuhakikisha kwamba, vitendo vya aibu kiasi hiki havijirudii tena ndani ya Kanisa kwa siku za usoni.

Dhamana ya kuwalinda watoto “Minorum tutela actuosa” inalenga kuwapatia watoto uhakika wa makuzi yao kiroho na kimwili mintarafu utu na heshima ya binadamu, kwani haya ni mambo ambayo yanafumbwa kikamilifu katika ujumbe wa Injili ambao Watoto wote wa Kanisa wanahamasishwa kuutangaza na kuushuhudia mbele ya watu. Kwa kuchapisha Katiba ya Tume ya kulinda watoto wadogo, tayari, sheria imeanza kutumika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.