2015-05-09 17:32:00

Kanisa limepiga hatua kubwa katika kudumisha majadiliano ya kidini


Kanisa Katoliki linatambua na kuheshimu mchango wa Wayahudi katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na maendeleo makubwa tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa majadiliano ya kidini, Nostra Aetate. Kanisa linakiri kuwa wokovu wa Kanisa umeaguliwa katika Maandiko Matakatifu, pale Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo alipofunga Agano la kale kwa njia ya watu wake. Kanisa linalishwa katika shina la Mzeituni ule mwema, ambapo matawi ya Mzeituni mwitu, yaliyo mataifa ya wapagani yamependakizwa juu yake.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sektretarieti ya uchumi Vatican wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Makardinali, Maaskofu na wanachama wa Chama cha Kitume cha Ukatekumeni mpya, katika mkutano wa kimataifa uliofanyika mjini Galilaya, nchini Israeli kwa kuwashirikisha pia Marabbi wa Kiyahudi. Imekuwa ni fursa ya pamoja kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50 ya Waraka wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano ya kidini na kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kumalizika kwa mauaji ya Wayahudi.

Mauaji haya yamekuwa ni chanzo cha magumu kwa watu wengi, changamoto na mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani kwa kukumbatia Heri za Mlimani, muhtsari wa Mafundisho makuu ya Yesu pamoja na kumwilisha Amri za Mungu katika maisha yao, chemchemi ya ukweli na maisha.

Njia ya Ukatekumeni mpya anasema Kardinali Pell ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; waamini wanaojikita katika kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko anakithamini sana chama hiki kutokana na utume wake, unaojikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwani kwa hakika wao ni kielelezo cha baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu wengi wanaelemewa na upweke hasi, wanataka kusikiliza ujumbe wa upendo ukitangazwa masikioni mwao, ili kupyaisha tena imani yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.