2015-05-09 12:05:00

Jumanne, Siku ya Dunia ya Wauguzi


Wauguzi duniani kote, watasherehekea  Siku ya Dunia  ya Wauguzi, Jumanne ijayo. Adhimisho la kila mwaka  tarehe 12  Mei, ambayo ni  siku ya kuzaliwa Florence Nightngale,  mwanzilishi wa huduma za uuguzi. Baraza la Kimataifa la Wauguzi, limetangaza Kaulimbiu ya adhimisho la mwaka huu kuwa, Wauguzi:Nguvu ya mabadiliko,ufanisi wa huduma kwa binadamu kwa gaharama nafuu. Maadhimisho ya siku hii, yanatajwa kuwa na umuhimu wake kutokana na umuhimu ya huduma hii inayogusa maisha ya kila binadamu. Kila mwaka hufanikisha kupitia mipango mbalimbali inayoandaliwa na wauguzi  mahalia. Kati ya yatakayofanyika  mwaka huu, ni pamoja na usambazaji wa majarida ya elimu na habari kwa  umma, juu ya huduma ya  wauguzi mahali popote duniani.

Kwa ajili ya mwaka huu , tayari Baraza la Dunia la Wauguzi , limekwisha sambaza mabango yenye  kuonyesha huduma ya muuguzi, kwa ajili ya kutoa ufahamu zaidi wa huduma za wauguzi katika maisha ya kijamii. Mabango yaliyotundikwa sehemu mbalimbali na vyama vya wauguzi kitaifa duniani kote.  Waandaaji wa tukio hili katika ngazi ya kimataifa wanahimiza  wauguzi kila mahali, kufanikisha upanuzi wa huduma za Wauguzi, kama Nguvu ya kuleta  mbadiliko, katika ufanisi wa  huduma  kwa binadamu  anayeteswa na maumivu.

Katika baadhi ya mataifa , adhimisho hili hufanyika kwa muda wa wiki moja  kitaifa,ili kumulikia zaidi  umuhimu wa huduma za wauguzi , kama ilivyo nchini Tanzania mwaka huu wanalenga zaidi katika huduma za wakunga , katika kupunguza vifo vya watoto wachanga na wakina mama wajawazito.

Kwa  mujibu wa Shirika lisilo la kiserikali la « Evidence4Action », watoto 47,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaofariki dunia kila mwaka Tanzania, nusu ya vifo hivyo hutokea wakati wa kuzaliwa. Na kwamba licha ya Tanzania kupiga hatua kubwa kwa kutimiza lengo la Maendeleo ya Milenia namba 4 la kupuguza vifo vya watoto wachanga, bado kuna watoto wanaopoteza maisha kutokana na huduma mbovu za afya ya uzazi. 








All the contents on this site are copyrighted ©.