2015-05-08 07:21:00

Wasaidieni vijana kupata utimilifu wa maisha kwa mwanga wa Injili


Viongozi wa utume wa vijana kwenye Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawasaidia vijana kupata utimilifu wa maisha yao mintarafu mwanga wa Injili pamoja na uwajibikaji makini katika maisha yao. Wanafunzi wanapaswa kuwajibika katika mchakato wa maisha kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha mambo msingi katika maisha, kanuni maadili na utu wema. Haya ni kati ya mambo ambayo yametiliwa mkazo wakati wa kongamano la kimataifa lililoandaliwa hivi karibuni na Tume ya Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya na kuratibiwa na Askofu mkuu Marek Jedraszwski, wa Jimbo kuu la Lodz, nchini Poland.

Kardinali Zenon Grocholewski, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki alishiriki na kutoa mada kuhusu umuhimu na dhamana ya elimu inayotolewa na Mama Kanisa katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Kongamano hili limefanyika wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume: Injili ya Uhai, Evangelium vitae, kunako mwaka 1995. Tangu wakati huo hadi leo hii kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza kiasi cha kutishia Injili ya Uhai, changamoto kwa vijana kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, hususan Barani Ulaya.

Wajumbe katika kongamano hili wanawataka vijana kuwajibika barabara katika maamuzi na maisha yao ya kila siku, sanjari na kuwasaidia vijana wenzao kuwa kwelini wadau wa Injili ya Uhai, kwa kuwashirikisha tunu msingi za Kiinjili. Kwa njia ya mwanga wa upendo na huruma inayofumbatwa katika maisha na utume wa Yesu Kristo, vijana wanaweza kuwajibika barabara katika maisha yao. Itakumbukwa kwaba, maisha ya chuo kikuu na kwenye taasisi za elimu ya juu, ni kipindi cha majaribu na changamoto nyingi za maisha, hapa mwanafunzi asipokuwa makini anaweza “kwenda na maji” wanasema wajumbe!

Huu ni wakati wa kujenga na kuimarisha maisha ya kiroho na kiutu kwa kuondokana na tabia ya ubinafsi na mawazo mepesi mepesi yanayowafanya vijana wengi kuwa ni watumwa wa mitandao ya kijamii na matokeo yake, wengi wao wanakengeuka na kujikuta wamemezwa na malimwengu, kiasi cha kushindwa kujishikamanisha na Mungu. Walezi wa vijana wanayo dhamana ya kuwasaidia vijana hawa kufungua akili, mioyo na mawazo yao kwa Mwenyezi Mungu, Kristo na Kanisa lake, ili kweli kipindi cha masomo Chuo kikuu na kwenye taasisi za elimu ya juu kiweze kuwa ni muda wa kujitajirisha: kiakili, kiroho, kimwili, kimaadili na kijamii kwa kujenga na kuimarisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu.

Ushuhuhuda makini unaotolewa na waamini katika maeneo yanayozunguka Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ni muhimu sana katika makuzi ya vijana wanaosoma vyuo vikuu. Kumbe, walimu na walezi wawasaidie vijana kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu anayezungumza na vijana kutoka katika undani wa maisha yao sanjari na kuwasaidia kuimarisha utashi na mawazo yao.  Walezi wawasaidie vijana kutambua umuhimu wa maisha ya Kijumuiya, ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa kama Wakristo, kwa kuwajibika katika maisha binafsi, jamii na katika dunia inayowazunguka.

Walimu na walezi wawe ni mashuhuda wa mang’amuzi ya mahusiano yao na Kristo pamoja na Kanisa lake, kwani vijana wanataka kuona mashuhuda na wala si Maprofessa wanaojikita katika nadharia peke yake; bali mashuhuda wanaothubutu kumwilisha kile ambacho wanafundisha na kukiamini. Vijana wanataka kuona ushuhuda unaojikita katika ukweli na maadili. Kimsingi haya ndiyo mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya kuwasaidia walimu na walezi kuwafunda vyema wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili kuwajibika kikamilifu katika maisha kwa njia ya ushuhuda dhidi ya utamaduni wa kifo unaotishia Injili ya Uhai.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.