2015-05-08 16:06:00

Rafiki mwema ni dhahabu!


Watu wawili wasiofahamiana, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume wanajikuta kwenye bustani ya mapumziko na wakiwa wamekalia dawati moja. Yule mwanamke alikuwa anasoma sehemu ya maandiko katika Biblia (habari ya Yona) na baada ya muda yule mwanaume akamuuliza yule mwanamke – unaamini kuwa kweli Yona alikaa katika tumbo la samaki kwa siku tatu? Yule mwanamke akamjibu – Biblia inatuambia hivyo. Na kama si kweli hivyo? Anauliza yule mwanaume. Nitamwuliza yeye Yona tutakapokutana mbinguni. Akajibu yule mwanamke. Na kama hayuko huko? Anaendelea yule mwanaume. Basi utamwuliza wewe. Anajibu yule mwanamke.

Hapa tunaona haja ya imani kubwa na iliyo na msingi imara. Bahati mbaya tunataka tujue kila kitu hasa kinachomhusu Mungu, na mbaya zaidi tunataka tujue tunavyotaka sisi.

Meister Eckhart anasema baadhi ya watu wanataka kumwona Mungu kwa macho kama wanavyomuona ng’ombe na kumpenda Mungu kama wanavyopenda ng’ombe wao kwa kiasi cha maziwa, jibini na faida wanayoipata toka kwa ng’ombe huyo.

Pengine namna hii ya kufikiriau kuelewa ndiyo inaweza kuwa sababu au kikwazo kwa imani ya wengi. Je ufahamu wetu wa kile alichofanya Kristo ukoje? Je mahusiano yetu na Kristo yakoje? Bwana na mtumwa au rafiki na rafiki? Wakati mwingine mtazamo uko wa bwana na mtumwa na kwa kweli katika aina hii ya urafiki, uhusiano unakita zaidi kwenye woga. Wenye uhusiano wa kiurafiki, ukaribu unakuwepo. Yesu anasema mwenyewe – Yoh. 15, 15 – siwaiti tena watumwa, kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu, nimewaarifu.

 Kwa maelezo haya yaonekana wazi jinsi Bwana Yesu anavyotaka uhusiano wetu uwe. Maisha ya ukristo yatuita katika ukuaji, tunapoaanza maisha ya imani – uhusiano wa mtumwa na bwana unaonekana lakini kadiri tunavyozidi kukua na kukomaa katika imani mahusiano yetu yanabadilika, yanajengeka mahusiano ya kirafiki kwa vile tunashirikishwa pia siri za ufalme wa Mungu.  Injili ya leo yatupa changamoto kubwa kuangalia imani yetu na ukomavu wetu kama unavyoonekana katika mapendo kati yetu, mahusiano yetu na ushirikiano wetu.

Ni kwa kiasi gani tunaifahamu hiyo siri ya Mungu ambayo Kristo ametufunulia? Kiasi kwamba tunakuwa rafiki zake Kristo? Hakika ufahamu wa kina wa Kristo ni nani na kile alichofanya kwa ajili yetu ungegeuza mahusiano yetu na Mungu Baba na pia maisha yetu ya ushuhuda – Yoh. 15,7 – ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo nanyi mtatendewa. Pia tunasoma katika Yoh. 15,16 – si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa, ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Hakika Mwenyezi Mungu anategemea na anatarajia makuzi toka kwetu. Kama vile mtoto azaliwavyo na kukua vivyo hivyo nasi tuna changamoto ya kukua na kuendelea mbele katika ushuhuda wa imani yetu.

Hii ofa ya urafiki wa Mungu kwetu ituwajibishe na kutufikirisha sana. Eti Mwenyezi Mungu anakuwa rafiki yetu. Sote twajua sifa za urafiki. Waswahili husema - akufae kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Wafaransa husema – rafiki mwaminifu ni taswira ya Mungu. Waitaliani husema – ampataye rafiki mwema amepata dhahabu. Hii ni baadhi tu ya mifano inayojaribu kuonesha umaana na umuhimu wa urafiki. Urafiki wa kweli hudumu, hubaki, hukua na kuzaa matunda - kama tunavyosoma kutoka Yoh. 15,7 – tunaalikwa tukae ndani yake Kristo na kuzaa matunda.

Huweza kutokea pia baadhi ya rafiki wakakosa uaminifu, wakachezea urafiki huo kwa ajili ya faida yao wenyewe. Namna kuu ya kujibu upendo huo wa Mungu kwetu ni kubaki katika pendo lake. Maana yake kutimiza mapenzi yake Baba – Yoh. 15,14 – ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Kuwa rafiki wa kweli wa Mungu ni kutimiza amri zake. Imani ya mama yule katika mfano itufikirishe sana – anaamini na hana wasiwasi juu ya ukuu wa Mungu. Ana uhakika wa kwenda mbinguni na ndiyo maana anaweza kujibu wazi kwamba Yona alibaki katika tumbo la samaki na anasema kwa uhakika kuwa jibu kamili atalitoa atakapokutana naye ana kwa ana. Yule mama ana uhakika wa kwenda mbinguni. Mara nyingi kuwa na wasiwasi na mashaka au kutokujiamini katika maisha kunasababisha kukosa mwelekeo mzuri katika utendaji wetu.

Yesu anatuambia leo kaeni katika pendo langu. Hakika ni mwaliko mtakatifu na mwaliko unaotuwajibisha sana. Katika somo II - 1Yoh. 4,8 tunasoma hivi; - yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Kwa kifupi upendo wa kweli watoka kwa Mungu. Mwenye kupenda kweli na vizuri ni lazima amjue na kumpenda Mungu kwanza. Sisi wanadamu tunashiriki utukufu na ukuu wa Mungu kwa neema. Sisi sio Mungu. Mungu ni pendo. Hali yake ni pendo. Pendo lake kwetu sisi ni zawadi. Mwanadamu anaalikwa kupokea zawadi hii na kuiweka au kuiishi katika maisha yetu na mahusiano yetu. Kwa njia yake Kristo sisi tumeshirikishwa pendo lake Mungu. Tunayo amri, wajibu na kila sababu ya kuambukizana pendo hili la Kimungu kati yetu. Huo ndiyo mwito wa Kristo leo.

 Pendo ni tendo linaloendana na mvuto lakini unaotuwajibisha. Ni mvuto unaoona kitu fulani kizuri na kuelekea kitu hicho. Lakini ni mvuto kwa kitu kinachofaa na kizuri. Nioneshe matendo yako nami nitajua imani yako. Kila mtu anapenda kile anachovutwa nacho. Injili ya leo yatualika kupenda kama Mungu alivyotupenda sisi. Upendo wa Mungu huleta uzima, huokoa, hutudai nasi pia tupendane kati yetu.

Mtume Paulo katika Rum. 13,8 – anasema – msiwiwe na mtu cho chote isipokuwa kupendana, kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.

Kristo anatupa amri ya kupendana kweli kweli. Je mapendo yako yakoje? Mapendo ya kweli ya Kristu hayana malipo. Mara nyingi tunapenda mtu kwa jinsi alivyo, kwa kile alichonacho au kwa kile afanyacho? Mafundisho ya kawaida na halisi yatudai tumpende mtu kwa jinsi alivyo. Lakini katika maisha yetu ya kawaida twaona kuwa mtu hupendwa kwa kile alicho nacho au kwa kile afanyacho. Huu ni upendo unaoangalia upande mmoja, uliojaa ubinafsi, upendo kupe. Hapendwi mtu bali yapendwa pochi yake. Kuchuna. Tamaa ya vitu inaongoza vionjo vyetu na si ukweli wa maisha. Tabia ya kuhangaikia na kuchangamkia mambo yanayopita tu. Kushikilia mambo ya juu juu kama mwewe na kuusahua ukweli halisi wa maisha. Bahati mbaya ndiyo falsafa iliyoikumba jamii yetu. Na ndivyo wengi wetu wanavyoishi.

Kwa maelezo na mafundisho ya Kibiblia mapendo  ni  kitambulisho halisi cha wanafunzi wa Yesu – Yh. 13,35  - hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.

Kitokacho mbinguni ni kitakatifu. Ni lazima kienezwe duniani kote. Pendo la Mungu linakuja kwetu kwa njia ya Mwanawe. Mwana naye anaeneza pendo hilo kwetu. Sisi tunalipeleka kwa wenzetu.  Haya basi nawaamuru ninyi, mpate kupendana. Ndivyo ilivyo katika Injili leo. Tendo la kupenda au kupendana kati yetu sisi wafuasi wake Kristo ni amri na si hiari. Tumesikia katika Injili mafundisho ya Yesu juu ya amri yangu. Ni ipi hiyo? Jibu lake liko wazi katika somo lenyewe la Injili ya leo. Amri yangu ndiyo hii – mpendane kama nilivyowapenda ninyi. Naye Mtume Paulo anakazia mwaliko katika Rum. 13,8 – akisema – msiwiwe na mtu cho chote isipokuwa kupendana, kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.

Tumsifu Yesu Kristo. 

Na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.