2015-05-08 09:19:00

Nendeni mkapige kura; dumisheni majadiliano, haki na amani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawaalika waamini na wananchi wa Burundi kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo mwaka huu 2015, ili kupata viongozi watakaochaguliwa na wananchi. Hali ya kisiasa nchini Burundi kwa sasa ni tete kutokana na maandamano ya wananchi wanaopinga Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena Urais kwa awamu ya tatu mfululizo, jambo ambalo wanasema ni ukiukwaji wa Katiba.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi katika ujumbe wao kwa Familia ya Mungu nchini Burundi, wanaonesha hali ya wasi wasi na mashaka makubwa kutokana na vurugu zinazoendelea nchini humo kiasi cha kusababisha mauaji na majeruhi wengi. Wananchi wengi wameyakimbia makazi yao kwa hofu ya kushambuliwa na kwamba, kuna wasi wasi wa kuzuka tena vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Maaskofu wanawataka wale wote wenye dhamana katika vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira ya haki na usalama, ili wananchi waweze kutekeleza dhamana ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Wale wanaowania uongozi wahakikishiwe usalama wa maisha yao na kupata fursa ya kuzungumza na wananchi katika uhuru kamili. Wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi, wapatiwe ulinzi wa kutosha, ili hatimaye, waweze kurejea tena majumbani mwao.

Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe kuhusu uvumi unaoendelea kusikika kwamba, vijana wa Chama tawala wamegawiwa silaha ili kuendesha vurugu na mauaji, kama uvumi huu ni kweli, basi vyombo vya ulinzi na usalama viwashughulikie kisheria, ili kuwajengea waamini amani na utulivu, ili uchaguzi uweze kuwa huru na wa haki badala ya kugubikwa na vurugu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi kwa namna ya pekee, linapenda kukazia mchakato wa majadiliano yaliyofanikisha Mkataba wa Arusha na hivyo kusitisha vita ya wenyewe kwa wenye iliyodumu kwa zaidi ya miaka kumi. Viongozi wakumbuke kwamba, uongozi ni huduma kwa ajili ya wengi, kumbe, si wakati wa kutafuta mafao binafsi au kwa ajili ya makundi ya watu. Kiongozi akubali kuwa ni Baba wa Taifa, anayejisadaka kwa ajili ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka vijana kukataa kishawishi cha kutumiwa na baadhi ya wanasiasa ili kufanya vurugu nchini Burundi. Wanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Burundi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.