2015-05-08 14:34:00

Mtumishi wa Mungu Kard. Mindszenty ni kielelezo cha Kanisa linaloteseka


Miaka 40 imekwishagota tangu Kardinali Jozsef  Mindszenty alipofariki dunia na kwamba, Kanisa limekwisha anzisha mchakato wa kutaka Mtumishi huyu wa Mungu atangazwe kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Tarehe 7 Mei 2015, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Mtumishi wa Mungu Jozsef alipofariki dunia.

Tukio hili limekwenda sanjari na Jubilei ya miaka 100 tangu alipopewa Daraja takatifu la Upadre na Miaka 75 ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom, Hungaria. Matukio yote haya yanaonesha upendo wa Mungu ambao umedhihirishwa na Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka katika wafu, mwaliko na changamoto ya kuendelea kushikamana na Yesu kwa kushika amri zake, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Ni kiongozi aliyeshuhudia mateso na mahangaiko ya watu wakati wa Vita kuu ya kwanza ya Dunia, akaonesha ujasiri mkubwa wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia, kwa kuwahudumia waamini kwa moyo mkuu na sadaka. Alipokuwa anaombea amani, akatiwa mbaroni na kuonja adha ya gereza, lakini moyoni mwake, alitamani kuwa ni Mchungaji mwema, anayeyamimina maisha kwa ajili ya Kondoo wake. Akawaimarisha ndugu zake katika imani, ili kukabiliana madhulumu ya Kikomunisti kwa ujasiri na imani kuu.

Licha ya magumu yote haya, lakini aliweza kudiriki kuanzisha mchakato wa Uinjilishaji nchini Hungaria, akikazia upendo kwa Mungu na jirani; Ibada kwa Bikira Maria, Mtakatifu Stefano na Watakatifu wengine kutoka Hungaria. Kunako mwaka 1948 akatiwa tena mbaroni kwa tuhuma za kutaka kupindua Serikali ya Kikomunisti na kupewa kifungo cha maisha gerezani.

Katika mazingira kama haya anasema Kardinali Pietro Parolin, akawa ni kielelezo cha Kanisa linalodhulumiwa, linaloteswa na kuzalisha mashuhuda na waungama imani. Ukuta wa Berlin, umeangushwa, lakini hata leo hii bado kuna watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na ukosefu wa misingi ya haki na amani. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kuombea amani na kumwilisha huruma kwa wote wanaoteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mateso na mahangaiko ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni mbegu ya Wakristo wapya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.