2015-05-08 14:21:00

Majadiliano katika upendo na udugu yanajenga na kuliimarisha Kanisa


Roho Mtakatifu akikubaliwa na kupokelewa kwa moyo wa sala na majadiliano ya kina, analiwezesha Kanisa kujenga umoja na mshikamano, kama ilivyotokea wakati wa mpasuko na migawanyiko katika Kanisa la mwanzo Mitume wa Yesu wakaonesha ujasiri wa kumsikiliza Roho Mtakatifu na hatimaye, umoja, upendo na mshikamano vikatawala tena miongoni mwa waamini. Haya ni majadiliano ya kidugu yaliyosaidia kukamilisha Mtaguso mkuu wa kwanza wa Yerusalem, uliojadili kwa kina na mapana kinzani na magumu yaliyowakumba Wakristo wa kwanza.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 8 Mei 2015 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema hapa kuna Wakristo waliokuwa wamejisimika katika Sheria na walitaka kuwashinikiza watu ambao walikuwa wameongokea Ukristo kufuata Sheria za Kiyahudi, lakini wakakutana na upinzani uliotolewa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, aliyelisaidia Kanisa la mwanzo kupembua matatizo na changamoto hizi kama ndugu wamoja katika Kristo na wala si kama adui.

Baba Mtakatifu anasema, hivi ndivyo waungwana wanavyosuluhisha matatizo na changamoto za maisha, kwa kutojishikamanisha na madaraka kwa nguvu, bali wanatafuta muafaka kwa njia ya sala na kwamba, matokeo yanatia moyo na kuwaachia aibu wale wote wanaopandikiza mbegu ya upinzani na migawanyiko. Pale ambapo kuna matatizo ambayo yanaonekana kutopatiwa ufumbuzi wa kudumu, Baba Mtakatifu anaonesha shaka ikiwa kama kweli hapo yupo Roho Mtakatifu.

Pale ambapo ndugu wanasalitiana ni dalili kwamba, hapa hayupo Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anasaidia kuwafundisha wanafunzi wa Yesu, ili hatimaye, waweze kushikamana kwa pamoja, si kwa kutekeleza mapenzi yao, bali umoja huu unapata chimbuko kutoka katika undani wa waamini wenyewe, wanaotaka kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.