2015-05-08 10:01:00

Kongamano kuhusu umuhimu wa familia katika mchakato wa maendeleo!


Familia ina umuhimu wa pekee sana katika maisha ya binadamu, kwani hapa ni chimbuko la la uhai na mapendo ambamo watoto wanazaliwa na kukua; ni mahali pa mtu kujisadaka kwa ajili ya mafao ya wengine; ni mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa; kuhusu dhana ya ukweli na uzuri. Familia ni Jumuiya ya asili, ambamo mahusiano ya jamii kiutu yanastawi na kudumisha umoja na mshikamano. Familia ipo kwa ajili ya familia yenyewe na wala si vinginevyo. Familia ni kiini cha jamii, kumbe inapaswa kiuheshimiwa na kuthaminiwa, ili iweze kutekeleza dhamana na majukumu yake.

Kwa kutambua ukweli kwamba ni katika familia ambamo ukuaji na maendeleo ya mwanadamu vinapata chimbuko lake, mchakato wa kudumisha misingi bora ya familia ni jambo la kupewa kipaumbele cha pekee katika hatua mbali mbali za maendeleo, Askofu mkuu Berndito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, ameandaa Kongamano maalum litakalofanyika hapo tarehe 14 Mei 2015, linaloongozwa na kauli mbiu “Familia na Maendeleo endelevu”. Huu ni utangulizi wa maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, mwezi Septemba 2015, tukio ambalo Baba Mtakatifu Francisko, anatarajiwa kushiriki kwa ukamilifu zaidi, ili kuhamasisha Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai.

Familia thabiti na makini, zinawezesha watoto wao kupata elimu makini, uzoefu wa mang’amuzi thabiti, tabia na mahusiano mema na jirani na kwamba, mara nyingi ni watu wanaopata mafanikio makubwa katika maisha na hivyo kusaidia kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii. Haya ni kati ya mambo ambayo yanatarajiwa kupembuliwa kwa kina na mapana na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia pamoja na wageni mashuhuri kutoka Umoja wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.