2015-05-08 14:50:00

Kard. Sandri: Mtakatifu Nicola ni kielelezo cha upatanisho wa Makanisa


Mtakatifu Nicola wa Bari ni alama ya upatanisho kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi, changamoto kwa Wakristo wote kukumbatia na kupenda kujenga na kukuza umoja wa Kanisa ili wote waweze kukua na kukomaa ndani ya Kristo, dhamana na wajibu ambao Wakristo wanapaswa kuuomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wakristo wanaweza kuendelea kumheshimu Mtakatifu Nicola kwa kuwa kweli ni watoto wapendwa wa Mungu na mawe hai katika ujenzi wa Kanisa la Kristo, tayari kumwachia Mungu nafasi katika maisha na vipaumbele vyao. Wakristo wawe wanyenyekevu katika kumfuasa Yesu; kielelezo cha huduma ya Kristo kwa watu wake; wakweli na watu wenye huruma, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, wakati wa maadhimisho ya kuhamisha Masalia ya Mwili wa Mtakatifu Nicola kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicola, Jimbo kuu la Bari, Italia, Ijumaa, tarehe 8 Machi 2015. Mtakatifu Nicola amekuwa kweli ni alama ya matumaini na neema ya urafiki kati ya Mungu na binadamu; kielelezo cha kiu ya umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu ni mchakato wa kumwilisha  Fumbo hili katika maisha ya waamini, ili kweli waweze kuwa ni Mkate unaomegwa kwa ajili ya wengine. Bahari ambayo ilikuwa ni kielelezo cha kifo, lakini kwa Mtakatifu Nicola, ikawa ni kielelezo cha ufufuko na maisha mapya yanayosimikwa katika upendo. Hii ni nafasi ya kuwakumbuka na kuwaombea wadau mbali mbali wanaoendelea kufanya kazi zao usiku na mchana ili kuokoa maisha ya maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wanaopambana uso kwa uso na kifo kwenye Bahari ya Mediterrania.

Waamini wawe na ujasiri wa kutambua ukuu na uzuri wa Injili wanayoiungama na kuimwilisha katika maisha. Yesu anayetembea juu ya maji ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na ubaya, mwaliko kwa waamini kumwachia Yesu Kristo, ili kweli aweze kuwa ni Bwana na Mwalimu katika hija ya maisha yao ya kila siku; tayari kung’oa ndago za dhambi, ubinafsi pamoja na hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.