2015-05-07 12:00:00

Upendo unamwilishwa katika matendo ya huruma na Heri za Mlimani


Upendo wa dhati na wa kweli unajidhihirisha katika matendo yanayogusa undani wa mtu na kuacha chapa ya kudumu. Yesu anawakumbusha wafuasi wake, kwamba, wale wote wanaotaka kuingia katika Ufalme wa Mungu hawana budi kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni pamoja na kuzishika Amri zake, zinazomwilishwa katika maisha adili na matakatifu. Upendo ni tendo endelevu katika maisha ya mwamini na wakati mwingine unakumbana na vizingiti, kama ilivyokuwa kwa Yesu kuubeba na hatimaye, kufa juu ya Msalaba, kielelezo cha upendo wa dhati.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Mei 2015 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Anasema, upendo unamwilishwa katika matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Yesu anaonesha mkazo huu katika mafundisho yake ya Heri za Mlimani na vigezo vitakavyotumika wakati wa hukumu ya mwisho.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mungu yuko kati ya watu wake na wala si kama walivyodhani wazushi wa mwanzo kwamba, Mungu yuko mbali sana na binadamu. Upendo wa Mungu unajidhihirisha kwa namna ya pekee kwa kumtuma Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo ili kuja kumkomboa mwanadamu. Upendo unajionesha kwa kushirikiana na wengine na wala si kwa kujitenga kama inavyojionesha katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni mwaliko pia kwa watawa wa ndani na wakaa pweke, wajitahidi kuwaonjesha upendo wale wote wanaowaendea kutaka ushauri.

Kukaa na kudumu katika upendo wa Yesu ni mchakato unaomwezesha mwamini kuwasiliana na kujadiliana na Mungu pamoja na jirani. Dhamana hii ni pevu, kutokana na ukweli kwamba, ubinafsi una mvuto mkali zaidi kiasi cha kuwafanya waamini kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake yote haya, ili waweze kupata utimilifu wa furaha, kwa kubaki na kuendelea kushikamana naye. Ni furaha inayoandamana na Fumbo la Msalaba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.