2015-05-07 09:10:00

Ombeeni haki na amani; umoja na utakatifu wa familia na miito!


Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima kutoka Ureno, kuanzia tarehe 7 Mei hadi tarehe 30 Septemba 2015, inatembezwa katika Majimbo mbali mbali nchini Italia, ili kuhamasisha waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja kuombea miito mitakatifu kwani mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache.

Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima inatembezwa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, anapoendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 Oktoba hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa; kusali kwa ajili ya umoja, upendo, mshikamano na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwani masuala haya mawili ni sawa na chanda na pete. Kwa sasa kuna damu ya watu wengi wasiokuwa na hatia inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, bado waamini wanahamasishwa kusali kwa ajili ya kuomba amani, maridhiano, umoja na mshikamano kati ya watu.

Kwa namna ya pekee, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anawaalika waamini kutubu na kuongoka na kwamba, waamini waendelee kusali kwa ajili ya wongofu wa wadhambi, ujumbe endelevu kutoka kwa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima. Ni mwezi ambao pia waamini wanahamasishwa kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili pamoja na kutenga muda wa kufanya tafakari ya kina, kama alivyogusia Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 6 Mei 2015.

Mkazo mkubwa wakati wa kutembeza Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima ni kusali kwa ajili ya miito, kwani maisha na utume wa Wakristo yanajikita katika sala inayomwilishwa daima katika matendo. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufundisha kwamba, Kanisa linawahitaji mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili watakaojitosa kimasomaso bila kuogopa kumshuhudia Kristo kwa watu wa Mataifa. Hiha hii pia inahamasisha ari na mwamko wa Kimissionari sanjari na kuendelea na mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kushiriki katika ujenzi wa ufalme wa Mungu kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.