2015-05-07 15:54:00

Kanisa Katoliki Mali: Vipaumbele: Majadiliano, Utu wa mtu na Upatanisho


Kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; kusimama kidete kupambana na misimamo mikali ya kidini na utengano; kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo; kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki, amani, umoja na upatanisho wa kitaifa ni kati ya mambo msingi ambayo yametiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Mei 2015 alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Mali, wakati huu linapoendelea na hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Nchi ya Mali katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni inakabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali zinazojikita katika masuala ya kisiasa na kijamii; haki, amani na usalama; mambo ambayo wakati mwingine yamesababisha mtafaruku wa kijamii. Kutokana na kinzani hizi amani, maridhiano na mfungamano wa kijamii vimejikuta vikitoweka na hivyo kusababisha majanga makubwa katika nchi.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu Katoliki Mali kwa kuendelea kujenga na kudumisha ari, moyo na utamaduni wa majadiliano ya kidini, ambayo yamemwilishwa katika utekelezaji wa miradi ya pamoja kati ya Waislam na Wakristo; kwa kulinda urithi na utamaduni wa wananchi wa Mali, lakini kwa namna ya pekee kwa kulinda Maktaba ya Kimataifa ya Timbuktù, urithi wa dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu wanaporejea nchini Mali ambako kwa sasa kuna kinzani na machafuko ya kisiasa, kuwaonesha watu uwepo wake wa karibu. Anawataka kuendelea kusimama kidete kupambana na misimamo mikali ya kidini inayosababisha mipasuko na utengano wa kijamii. Hii ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi na hali ya watu kutafuta mafao ya binafsi na badala yake, waanze mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani pamoja na mafao ya wengi.

Wakristo pamoja na viongozi wao, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo mema na adili yanayobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili. Familia za Kikristo ziendelee kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mafundisho na Mapokeo ya Kanisa. Wakatae kishawishi cha ndoa za wake wengi na talaka; kwa kuheshimu na kuthamini utu wa mwanamke katika familia na jamii husika.

Familia za Kikristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Mali, wasimame kidete kupinga vitendo vya uvunjaji wa haki, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake kwa kutambua kwamba, Yesu aliwaheshimu wanawake, kiasi cha kukubali kutungwa mimba na kuzaliwa na Bikira Maria.

Huu ni mwaliko pia kwa Kanisa mahalia kuhakikisha kwamba, linajikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuleta mvuto hata katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kanisa nchini Mali, linahimizwa kuendelea kujikita katika mikakati na sera za kichungaji zinazopania kuwajengea wananchi uwezo wa kujiletea maendeleo endelevu pasi na ubaguzi wa kidini au kikabila, bali kwa kujikita katika utamaduni wa mshikamano wa kidugu, ukarimu pamoja na kukataa kishawishi cha kutumbia katika vurugu na badala yake, wawe ni vyombo vya kweli katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.