2015-05-06 08:34:00

Watoto wakifundwa vyema wanaweza kuwa ni wajenzi na vyombo vya amani


Zaidi ya watoto elfu saba, Jumatatu tarehe 11 Mei 2015 wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Hii itakuwa ni fursa kwa watoto hawa kuweza kungumza na Baba Mtakatifu kuhusu amani, upendo, ukarimu, urafiki na mshikamano wa kidugu. Hili ni tukio ambalo linaandaliwa na Kikundi kinachojulikana kama “ la Fabbrica di pace”, yaani waundaji wa amani. Lengo ni kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano, kwa sasa na kwa siku za usoni.

Tukio hili ambalo limezunduliwa Jumanne, tarehe 5 Mei 2015 na Maria Rita Parsi, Mratibu mkuu wa “la Fabbrica di pace” na kuhudhuriwa na wadau kutoka katika sekta ya elimu, wanasiasa, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa Kanisa kwenye Makao makuu ya Shirika la Kilimo na Chakula, FAO anasema, watoto ndio matumaini ya taifa na jeuri ya Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni, hawa wanapaswa kufundwa vyema ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani kwa kukataa kishawishi cha kutumbukia katika vita, kinzani na migogoro ambayo imekuwa na athari kubwa katika maisha ya watu wengi duniani.

Dhana ya amani, inapaswa kujengwa hatua kwa hatua, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali kuanzia katika familia, shule, njia za mawasiliano ya jamii, taasisi na wanasiasa, bila kuwasahau wanamichezo ambao wanayo nafasi kubwa katika kuhamasisha dhana ya amani kati ya watu. Ujenzi wa amani ni dhamana inayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa. Lengo ni kujenga na kukuza majadiliano yanayojikita katika maridhiano, ili kupata amani ya kweli.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amepokea mwaliko wa kukaa, kuzungumza na kucheza na watoto, kwa kutambua umuhimu wa malezi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani na maridhiano kati ya watu. Watoto wakijengewa mazingira bora wanaweza kuwa kweli ni vyombo vya amani, upatanisho, maridhiano, umoja, udugu na mshikamano wa kweli.

Dhana hii inaweza kuanza kujengeka katika familia na shule ambako watoto kutoka katika makabila, dini na mataifa mbali mbali wanakutana. Kwa njia hii wanaweza kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya amani. Baba Mtakatifu Francisko anahimiza mfungamano wa malezi kati ya watoto, familia na shule, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kuzungumza bila ya kuwekeana vizingiti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.