2015-05-06 14:57:00

Watanzania wawili watunza amani wauawa DRC


Askari wawili wa Watanzania , waliokuwa wakitumikia  Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wameuawa, wengine 13  kujeruhiwa, na wanne  hawajulikani walipo, baada ya kushambuliwa ghafla  mapema siku ya Jumanne , wakiwa katika lindo.  watu wanaodhaniwa kuwa waasi wanamgambo Kiislam wa Uganda,waliwashambulia askari hao,  Umoja wa Mataifa umetaarifu .

Felix Basse, Msemaji wa Tume ya Kulinda Amani inayojulikana kwa jina la MONUSCO, bila kutaja majina ya marehemu amesema, askari hao walishambuliwa  katika kijiji cha Kikiki,  kiasi cha  Km 50 (30 miles) Kaskazini mwa mji wa Beni, Kivu Kaskazini, mapema Jumanne. Na kwamba Jeshi la DRC, liliua waasi 16 wanamgambo wa chama cha Uganda Allied Democratic Forces (ADF), wakati wa mapigano makali  yaliyofanyika katika ukanda huo mwishoni mwa wiki.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  akithibitisha taarifa za kuuawa kwa Askari hao , amesema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani vikali mashambulizi dhidi  ya Walinzi wa Amani, wanayofanykazi kazi zao kwa dhamira ya kutoa ulinzi kwa raia. Na kwamba  juhudi za Umoja wa Mataifa kutetea raia wema hazitakatishwa tamaa na mashambulizi kama hayo lakini umoja huo , utachukua hatua zote muhimu kulinda raia na kusambaratisha  makundi ya waasi katika Mashariki mwa DRC.

 Na Mkuu wa Tume ya MONUSCO, Martin Kobler, akiwa wametiwa simanzi na tukio hili, anasema, hawatavumilia  tena ya mashambulizi haya mara kwa mara dhidi ya Watunza amani wilayani  Beni. Na sasa MONUSCO  itatekeleza  shughuli zaidi kwa uimara zaidi.

Na Rwanda yajihami na wingi wa wakimbizi tokea Burundi

Na taifa la Rwanda siku ya Jumanne lilionyesha kujali wingi wa wakimbizi wanaoingia Rwanda tokea Burundi , kufuatia maandamano ya upinzani nchini Burundi dhidi ya maamuzi ya Rias Pierre Nkuruzinza kutaka kugombea kiti cha Rais awamu ya tatu. Upinzani mkali ulianza baada ya Rais Pierre Nkurunziza  kutangaza nia yake ya kutaka kusimama katika uchaguzi wa Juni 26 kugombea kiti cha Rais,na hivyo kuitumbukiza Burundi katika mgogoro mpya wa  kisiasa, baada ya kuwa na utulivu na amani kwa takribani miaka kumi, baada ya kusitishwa vita ya wenye kwa wenyewe vilivyodumu  kati ya 1993-2005.

Habari inasema, kwa wakati huu ,Watu zaidi ya  24,000 wengi wao wakiwa Watutsi wamekimbilia Rwanda, kwa  hofu ya kuzuka kwa mapigano mengine ya kikabila, ambayo itakuwa ni kutonesha kovu la Rwanda, ambayo bado inalilia watu wake waliofariki katika  mauaji ya kimbari ya 1994, yaliyoua zaidi ya 800,000 Watutsi na Wahutu.  Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje , Louise Mushikiwabo anasema,  pamoja na kuheshimu sana  uhuru wa Burundi katika kushughulikia mambo yake ya  ndani, Rwanda inaona usalama wa watu wasio na hatia kimkoa,kikanda na kimataifa, unaweka hatarini.  Na hivyo wanatoa ombi kwa viongozi wa Burundi kufanya kila linalowezekana kurudisha hali ya utulivu na amani katika taifa lao .

Kwa mujibu wa taarifa za vyama vya kiraia na kijamii, tangu kuzuka kwa maandamano ya upinzani mitaani Burundi, wiki iliyopita,  watu 12 wameuawa, katika mapambano na polisi.  Siku ya Jumanne makundi madogomadogo ya upinzani yalirejea tena mtaani na polisi mabomu ya machozi na  mipira ya maji kusambaratisha waandamanaji. Katibu wa Nchi wa Marekani, John Kerry, akiitembelea Afrika, Jumatatu, mbele ya wanahabari, alimtaka Rais  Pierre Nkuruzinza  kuheshimu Katiba ya Burundi, kwani nia yake ya kutaka kutawala kwa awamu ya tatu ni moja kwa moja kukiuka katiba ya  Burundi katiba.

Wakimbizi Tanzania

Wakati huohuo taarifa zimetolewa kwamba, zaidi ya wakimbizi 4000 wa Burundi wameingia Tanzania, idadi kubwa ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto. Hllo limethibitishwa na Mwakilishi Mkazi wa Umoja  wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,  Alvaro Rodriguez,wakati akizungumza na  vyombo vya habari. Na kwamba kwa sasa wako katika mashauriano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi na wahisani ili kuongeza usaidizi wa huduma za msingi kwa wakimbizi hao ikiwemo chanjo  kwa watoto , ambapo serikali ya Tanzania imeshajadili suala la kutoa eneo la kujenga kambi nyingine,  iwapo idadi  ya wakimbizi itaongezeka zaidi.

Na Rais Jakaya Kikwete  wa Tanzania , kama Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Burundi ikiwa mwanachama wa Jumuiya hiyo,  amepeleka ujumbe wa mawaziri kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutathmini machafuko ya kisiasa Burundi. .

Taarifa kutoka Ofisi ya Rais iliyosambazwa katika vyombo vya habari na Mawasiliano, siku ya Jumanne, inasema Ujumbe huo utakutana na  wadau wote muhimu katika mzozo wa Burundi. Tume inatazamiwa kukamilisha kazi yake mwishoni mwa wiki. Na kwamba suluhisho la hali ya kisiasa inayoendelea  Burundi, linaweza tu kupatikana iwapo Burundi  itaheshimu  sheria  mama  za nchi na Sheria ya Uchaguzi. Rais Kikwete alieleza wakati akijibu swali katika mkutano wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu mjini New York.








All the contents on this site are copyrighted ©.