2015-05-06 07:54:00

Rais Raul Castro Ruz wa Cuba kutinga Vatican hapo tarehe 10 Mei 2015


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 10 Mei 2015 majira ya asubuhi, anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Raul Castro Ruz wa Cuba. Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican ameyabainisha haya, Jumanne, tarehe 5 Mei 2015 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana kwa faragha na Rais Raul ambaye hivi karibuni alimshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kusaidia sana mchakato wa kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Cuba na Marekani, nchi ambazo zimekuwa na uhasama kwa zaidi ya miaka hamsini.

Padre Lombardi anakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Cuba, Mwezi Septemba 2015 wakati atakapokuwa njiani kuelekea nchini Marekani, ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, kuhutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kumtangaza Mwenyeheri Fra Junipero Serra kuwa Mtakatifu. Serikali ya Marekani inaendelea kuboresha mchakato wa mahusiano ya kidiplomasia kwa viongozi wa nchi hizi mbili kuendelea kukutana na kuzungumza, ili hatimaye, kuweza kufikia muafaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.