2015-05-06 10:54:00

Mh. Padre Emery Kibal Manong'loo ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Kole


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Emery Kibal Mansong’loo kutoka Shirika la Mapadre wa Mateso, “Passionisti” kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kole, nchini DRC. Askofu mteule Mansong’loo aliwahi kuwa Mkuu wa Kanda ya Shirika la Mapadre wa Mateso, DRC. Tangu mwaka 2008 Jimbo Katoliki la Kole lilikuwa wazi kufuatia kung’atuka kutoka madarakani kwa Askofu Stanisla Lukumwena kutokana na machafuko ya kikabila jimboni humo.

Askofu mteule Emery Kibal Mansong’loo alizaliwa kunako tarehe 28 Juni 1969, huko Kimputu, Jimbo Katoliki la Idiofa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 31 Julai 1998 akaweka nadhiri zake za daima na kupewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 2 Agosti 1998, Jimbo kuu la Kinshasa. Tangu wakati huo amewahi kuwa ni Paroko msaidizi, Paroko na baadaye kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2005 alipelekwa kwa masomo ya juu na hatimaye, kujipatia Shahada ya uzamili katika Liturujia kutoka katika Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mt. Anselmi, kilichoko mjini Roma.

Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2013 amekuwa Mkuu wa Kanda ya Mapadre wa Mateso kwa awamu mbili, Jaalim na  mlezi wa baadhi ya vyuo vikuu nchini DRC. Kunako mwaka 2008 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Rais wa ASUMA. Mwaka 2011 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Mjumbe wa Uongozi Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Congo, Kinshasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.