2015-05-06 14:17:00

Mapambano dhidi ya ugaidi :Marekani na Somalia kushirikiana


Katibu wa Marekani John Kerry, wiki hii akitembelea  mataifa kadhaa ya Afrika, pamoja na  Kenya, Djibouti, Jumanne alitembelea Somalia bila kutarajiwa. Ziara yake Somalia imetajwa kuandika historia mpya kwa Katibu wa Nchi wa Marekani kuzuru Somalia mara ya kwanza, baada ya kupita kupita miongo miwili, tangu Maaskari wa Marekani walipouawa Kaskazini mwa Somalia na burutwa kikatili katika mitaa ya Mogadishu  katika mitaa ya Mogadishu, jambo lililoifedhehesha vibaya Marekani.  Hivyo John Kerry kukutana na uongozi wa serikali ya mpito ya Somalia, imekuwa ishara ya ukurasa mpya wa Marekani katika mahusiano yake na serikali ya Somalia inayoteswa  na  giza la ghasia za wenyewe kwa wenyewe. 

Ziara ya John Kerry mjini Mogadishu, imefanyika chini ya ulinzi mkali  kiasi kwamba, viongozi wengi wa Serikali ya Somalia, hawakuwa na taarifa kama Kerry, atajiunga na  Waziri wa Mambo ya  Afrika wa Marekani, Linda Thomas-Greenfield, kutembelea Afrika. Ajenda kuu katika majadiliano yake na Rais wa Serikali ya Mpito ya Somalia , ilikuwa kupambana na kikundi cha al shabab ambacho kina uhusiano wa karibu na kikundi cha kigaidi cha al Qaida , ambacho kimekuwa kitisho kikubwa kwa maisha ya watu wa Somalia na nchi jirani ya Kenya kwa zaidi ya miaka minane. Mwezi uliopita wanamgambo hao wa al Shabab walifanya shambulio la kinyama katika  Chuo Kikuu cha Garissa Kenya na kuuawa watu 148, wengi wao wakiwa wanafunzi.

Somalia imekuwa bila utendaji wa uhakika wa serikali Kuu, kwa miongo miwili na nusu, au tangu  wababe wa vita kuuagusha utawala wa kidikteta Siad Barre mwaka 1991, ikifutiwa na kusambaratika kwa umoja wa kitaifa, na taifa kubaki limegawanyika vipandevipande kikabila na kidini. Hata hivyo, kwa sasa kuna mabadiliko chanya kidogo baada ya kupitishwa kwa katiba mpya ya muda miaka mitatu iliyopita, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa na Umoja na Afrika. 

Bwana Kerry amesema , kwa kutambua mafanikio yaliyopatikana, serikali ya Marekani inaahidi  kuanza mchakato wa kuanzisha ujenzi wa  majengo kwa ajili ya ujumbe wake wa  kidiplomasia mjini Mogadishu,na  kwa ajili ya ufanikishaji wa msaada wa kuirejesha  Somalia katika maisha ya amani, ustawi na utulivu, kama mastahili ya watu wote  wa Somalia.

Kabla ya Somalia, John Kerry,  alikutana na viongozi wa ngazi ya juu nchini Kenya, ambako alifikisha rambirambi za  Rais Obama na Wamarekani wote, kufuatia tukio la shambulio baya la kigaidi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Garissa, mwezi uliopita, na pia kwa ajili ya matukio mengi yote ya kusikitisha ambamo watu wamekuwa wakipoteza maisha kama ilivyotokea huko Mandera , Wajir,  Mombasa na kwingineko . Amesema matukio haya badala ya kuwatenganisha watu wenye mapenzi mema,  huwaunganisha katika kiungo kilicho imara zaidi cha kutetea haki za binadamu, uadilifu, heshima  na amani.

Kerry  alizungumzia kwa kirefu juhudi za Marekani kama mshiriki wa ngazi ya juu katika kupambana na ugaidi . Na kwamba Kenya inahitaji msaada na mshikamano wa kimataifa , kukabiliana na ugaidi na kuhimili changamoto ya maelfu ya wakimbizi wanaoishi Kenya kwa wakati huu.  Jumatano hii , Kerry akiwa  nchini Djibouti , alikutana na Rais Ismail Omar Guelleh na Waziri Mkuu Mahamoud Ali Youssouf, ambamo katika mazungumzo yao , ameishukuru serikali ya Djibouti  kwa msaada wake, unaoiwezesha  Marekani kufanya shughuli zake. 

Na akirejea kinachoendelea Burundi, ametoa wito kwa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, afute nia yake ya kutaka kugombea awamu nyingine badala yake aheshimu Katiba ya nchi yake na Katiba ya uchaguzi, kwa ajili ya udumishaji amani na mapatano Burundi.  








All the contents on this site are copyrighted ©.