2015-05-06 15:18:00

Majina ya wenyeheri na watumishi wa Mungu watarajiwa


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Siku ya Jumanne, tarehe 5 Mei 2015 ameridhia waamini kumi na moja kuandikwa katika kitabu cha mchakato wa kuwatangaza kuwa wenyeheri baada ya kuridhika na sala pamoja na miujiza iliyofanywa kwa maombezi yao.

Mwenyeheri Junìpero Serra, aliyejulikana kama Michele Giuseppe Serra, aliyezaliwa nchini Hispania kunako tarehe 24 Novemba 1713 na kufariki dunia huko Monerrey, Marekani tarehe 28 Agosti 1784 anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu wakati wa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Marekani mwezi Septemba 2015. Papa ameridhia maamuzi yaliyofanywa na wajumbe wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, katika kikao chao cha hivi karibuni.

Wengine ni: Mwenyeheri Vincenzo Gross, Padre wa Jimbo na mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Vituo vya watoto, kutoka Italia, aliyezaliwa kunako tarehe 9 Machi 1845 na kufariki dunia tarehe 7 Novemba 1917. Mwenyeheri Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, aliyekuwa anajulikana kama Maria Isabela Salvat Romero, Mama mkuu wa Shirika la Watawa Msalaba, aliyezaliwa Madrid, Hispania tarehe 20 Februari 1926 na kufariki dunia tarehe 31 Okt9oba 1998.

Waamini wengine waliotambuliwa ni: Mtumishi wa Mungu Giacomjo Abbondo, Padre wa Jimbo, aliyezaliwa Italia, tarehe 27 Agosti 1720 na kufariki dunia huko Tronzano, Italia tarehe 9 Februari 1788. Kanisa limetambua ushuhuda wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Mario Borzaga, Padre na mwanzilishi wa Shirika la Watumishi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na wenzake: Paolo Thoj Xyooj, Mwamini mlei aliyeuwawa kutokana na chuki ya imani, huko Laos kunako mwaka 1960.

Kanisa limekiri ushujaa wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Giacinto Vera, Askofu wa Montevideo, aliyezaliwa kunako tarehe 3 Julai 1813 kwenye Mwambao wa Bahari ya Atlantic na kufariki dunia nchini Uruguay tarehe 6 Mei 1881. Mtumishi wa Mungu Antonio Antie, Padre na Mtawa Mkapuchini, aliyezaliwa huko Croazia tarehe 16 Aprili 1893 na kufariki dunia Zagabria, Croazia tarehe 4 Machi 1965. Mtumishi wa Mungu Giulia Colbert in Falletti di Barolo, mwamini mlei, mjane na mwanzilishi wa Shirika Mabinti wa Yesu Mchungaji mwema, aliyezaliwa nchini Ufaransa tarehe 26 Juni 1786 na kufariki dunia, Torino, Italia tarehe 19 Januari 1864.

Mama Kanisa ametambua ushuhuda wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Brigida Maria Postorino, muasisi wa Shirika la Watawa Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, aliyezaliwa Italia tarehe 19 Novemba 1865 na kufariki dunia mjini Frascati, Italia tarehe 30 Machi 1960. Mtumishi wa Mungu Raffaela Maria wa Yesu Ostia, aliyejulikana kama Raffaela Martinez Cavavate Ballesteros, mtawa wa ndani wa Shirika la Wakapuchini wa Mtakatifu Clara, aliyezaliwa Maracena, Hispania kunako tarehe 31 Machi 1915 na kufariki dunia nchini Hispania kunako tarehe 29 Mei 1991.

Kanisa limetambua pia ushuhuda wa imani uliooneshwa na Mtumishi wa Mungu Sergio Bernardini, Mwamini mlei, Baba wa familia, aliyezaliwa nchini Italia kunako tarehe 20 Mei 1882 na kufariki dunia huko Verica, Italia tarehe 12 Oktoba 1966. Mwishoni, Kanisa pia limetambua ushuhuda ulioneshwa na Domenica Bedonni in Bernardini, mwamini mlei, mjane na mama wa familia, aliyezaliwa huko Verica, Italia tarehe 12 Aprili 1889 na kufariki dunia akiwa huko Modena, Italia tarehe 27 Februari 1971.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.