2015-05-06 07:24:00

Jubilei ya huruma ya Mungu: Yatakayojiri wakati wa maadhimisho haya!


Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko ni kipindi muafaka kwa Wakristo kukimbilia huruma ya Mungu sanjari na kuendelea kujikita katika  mchakato wa Uinjilishaji mpya, toba, wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Hili ndilo lengo kuu la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, utakaozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015, kama kielelezo cha kufungwa kwa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka 50 iliyopita.

Mwaka Mtakatifu utafungwa rasmi hapo tarehe 20 Novemba 2016, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Haya yamefafanuliwa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumanne, tarehe 5 Mei 2015. “Iweni na huruma” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kanisa linaishi na linatamani kuwa daima ni chombo cha kugawa huruma ya Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake Injili ya Furaha. Ni maadhimisho ambayo yatafanyika mjini Roma na kwenye Makanisa mahalia, kwani kila adhimisho la Jubilei, lina lengo na namna yake ya kuadhimisha.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, waamini wataweza kuadhimisha pia tukio hili la huruma ya Mungu kwenye Makanisa mahalia, kwa kufungua malango ya huruma katika madhabahu au kwenye Makanisa makuu, yenye umuhimu wa pekee katika Makanisa mahalia. Ni Jubilei inayojikita katika maisha na utume wa Kanisa kama chombo cha ushuhuda wa huruma ya Mungu.

Katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, mwanzo wa kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2016, Baba Mtakatifu atawatuma rasmi “Wamissionari wa huruma ya Mungu”; kwenda sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwaondolea watu dhambi ambazo, kimsingi zinatolewa kwa idhini ya kiti kitakatifu. Hawa ni Mapadre wanyenyekevu, wenye uwezo wa kusikiliza na kufahamu udhaifu na mapungufu ya binadamu, tayari kuwaonjesha ile huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo mchungaji mwema.

Nembo ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imeandaliwa na Padre Marko Ivan Rupnik inayoonesha muhtasari wa huruma ya Mungu. Ni picha inayoonesha upendo wa Kristo unaobubujika tangu katika Fumbo la Umwilisho na kupata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Hii ni picha inayomwonesha Baba mwenye huruma anayemkumbatia Mwanaye mpotevu, kiasi cha kugusa undani wa maisha ya mtu na hivyo kumkirimia “cheche” za toba na wongofu wa ndani, tayari kugeuka na kuwa mtu mpya zaidi.

Askofu mkuu Fisichella anasema, waamini kwa namna ya pekee kabisa wanaalikwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanauishi Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma, kutohukumu wala kuwanyooshea wengine kidole, bali kusamehe na kuwakirimia msamaha na upendo usiokuwa na mipaka.

Kalenda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu: Baada ya udinduzi rasmi, kutafutia maadhimisho ya mwaka Mtakatifu kwa makundi ya watu mbali mbali. Kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21 Januari 2016, hii itakuwa ni fursa kwa waamini wanaojihusisha na ulimwengu wa mahujaji. Tarehe 3 Aprili 2016 ni siku maalum kwa ajili ya watu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika huduma inayojikita katika huruma ya Mungu.

Tarehe 24 Aprili 2016 itakuwa ni siku maalum kwa vijana walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, kuungama imani yao, tayari kuilinda na kuishuhudia katika uhalisia wa maisha. Tarehe 29 Mei 2016, Kanisa litaadhimisha Jubilei ya Mashemasi, ambao wamewekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya mapendo kwa Familia ya Mungu. Tarehe 3 Juni 2016 ni Jubilei ya Mapadre ambao kimsingi ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Tarehe 12 Juni 2016 ni Jubilei ya wagonjwa na walemavu.

Tarehe 4 Septemba 2016 ni siku maalum kwa wafanyakazi wanaotekeleza dhamana yao katika huduma ya kujitolea. Tarehe 25 Septemba 2016 ni Siku ya Makatekista, watu wanaojisadaka katika malezi na majiundo ya Familia ya Mungu. Tarehe 6 Novemba 2016, itakuwa ni Jubilei ya wafungwa, mkazo ni kutambua utu na heshima yao kama binadamu; watu wanaochangamotishwa kubadilika na kuwa wema zaidi baada ya kuhitimu adhabu yao gerezani.

Askofu mkuu Fisichella anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu, Maaskofu na Mapadre watapaswa kutenda matukio maalum yanaoonesha ile chapa ya huruma ya Mungu katika hija ya maisha ya watu. Ni fursa ya kuwaendea wale ambao wako pembezoni mwa jamii; kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wagonjwa na wale wanaoteseka kutoka na sababu mbali mbali za maisha, bila kuwasahau wahamiaji na wakimbizi. Matukio haya yanapaswa kufanyika pia kwenye Makanisa mahalia, kama kielelezo cha upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kweli watu wengi zaidi waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini na mahujaji watakaofika mjini Roma kama watu binafsi, watakuwa na nafasi ya kusali katika Makanisa maalum ambayo yametengwa kwa ajili ya kutoa huduma hii. Hapa wataweza kujiandaa kupita katika Mlango Mtakatifu baada ya kukamilisha mambo msingi yanayohitajika ili kupata rehema kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika matukio kama haya.Mtandao maalum wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa wale wanaotaka kupata habari zaidi wanaweza kutembelea mtandao ambao umefunguliwa kwa ajili ya kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema wanaotaka kweli kuikimbilia huruma ya Mungu kwa anuani ifuatayo:

www. Iubilaeummisericordiae.va

Au kwa anuani ifuatayo pia: www.im.va Hapa taarifa zinapatikana katika lugha saba za kimataifa, yaani: Kiingereza, Kiitalia, Kihispania, Kireno, Kifaransa, Kijerumani na Kipolishi. Mitandao mbali mbali ya jamii itaweza pia kutumika ili kuwajulisha watu mara moja matukio muhimu yatakayokuwa yanaadhimishwa na Mama Kanisa katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.