2015-05-06 09:20:00

Baada ya machafuko ya kisiasa Burundi: Anzeni mchakato wa majadiliano


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Barani Afrika, AACC kwa pamoja wametoa tamko linalowataka wananchi wa Burundi kumaliza machafuko ya kisiasa yanayoendelea kufuka moshi nchini humo kwa njia za haki na majadiliano badala ya fujo na vurugu kwani wanaweza kujikuta wanatumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Mabaraza ya Makanisa yanasikitishwa sana na uvunjifu wa amani unaoendelea kujitokeza nchini Burundi kutokana na mchakato wa uchaguzi mkuu 2015.

Tamko ambalo limetiwa sahihi na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Dr. Andrè Karamaga, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Barani Afrika, wanasema, machafuko haya ni ya aina yake kuwahi kutoka tangu mwaka 2005, Burundi ilipohitimisha vita ya wenyewe kwa wenyewe, iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Viongozi wa Makanisa wanaomboleza na wale ambao wamewapoteza ndugu na jamaa zao kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi na kwamba, wanawaomba wananchi wa Burundi, kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kupata ufumbuzi wa kudumu kabla mambo hayaharibika zaidi. Wanawaomba viongozi wa Makanisa nchini humo kuendelea kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani, usalama na maridhiano kati ya watu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na Baraza la Makanisa Barani Afrika, wanawaomba waamini wao pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea: haki, amani na usalama nchini Burundi.

Na Padre Ricahrd A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.