2015-05-05 09:07:00

Waamini nchini Canada kuandamana kutetea Injili ya Uhai dhidi ya kifo!


Chama cha Maisha na Familia, Ocvf, ambacho kiko chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada tarehe 14 Mei 2015 kimeandaa maandamano makubwa kwa ajili ya kuenzi Injili ya Uhai, yatakayoongozwa na kauli mbiu “ Tunaandamana katika mwanga wa Mungu”. Maaskofu wanabainisha kwamba, maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe yanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kutetewa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpoango wa Mungu.

 

Waamini wanaandama ili kutetea Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba.Maaskofu wanakumbusha kwamba, nje ya Mwenyezi Mungu, maisha ya binadamu yanageuzwa kuwa kama bidhaa inayoweza kuuzwa au kununuliwa dukani. Hizi ni dalili za kukengeuka na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema. Kuna haja ya waamini kusimama kidete kulinda na kutetea kazi ya uumbaji, hususan maisha ya binadamu ambayo kwa sasa yanashambuliwa na giza nene.

Kwa mwanga wa Injili, waamini wanaweza kusimama kidete kufanya maamuzi machungu kuhusu maisha, ili kutetea maisha ya mwanadamu. Kwa kujikita katika Injili, waamini wanakuwa na jeuri ya kujisadaka kwa ajili ya jirani zao; kwa kuwalinda na kuwatetea. Mwanadamu anapaswa kuishi kwa kuheshimu mpango wa Mungu katika maisha yake, kwani uha iwa binadamu una thamani kubwa, ndiyo maana waamini nchini Canada wanaandamana ili kweli Injili ya Uhai, iweze kutawala badala ya kumezwa na utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.