2015-05-05 10:09:00

Mihimili mikuu ya Uinjilishaji Mpya haina budi kufundwa barabara!


Mchakato wa Uinjilishaji mpya unahitaji majiundo makini na endelevu yatakayowasaidia waamini kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kwani: ushuhuda, maisha na utume wa Kanisa ni mambo msingi katika kufufua imani ndani na nje ya Bara la Afrika. Waamini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani katika uhalisia wa maisha yao sanjari na utamadunisho, vinginevyo, wanaweza kujikuta kwamba, imani inaelea katika ombwe pasi na kukita mizizi katika maisha, tamaduni na mila za watu husika.

Hizi ndizo changamoto ambazo hivi karibuni zimefanyiwa kazi na Kanisa Katoliki nchini Pwani ya Pembe, katika maadhimisho ya Kongamano la Kimissionari Kimataifa lililohudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Pwani ya Pembe. Ili Kanisa liwe kuwa na uhakika wa mchakato wa Uinjilishaji mpya kuna haja ya kuifunda mihimili ya Uinjilishaji, ili iweze kufahamu dhamana na majukumu yaliyoko mbele yao, tayari kuyafanyia kazi.

Kutokana na changamoto za Uinjilishaji mpya kuna haja ya kutambua kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya Injili, historia na tamaduni za watu, ili kweli Injili iweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Uinjilishaji na Utamadunisho ni changamoto kuu mbili zinazopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa Barani Afrika. Uinjilishaji mpya unatambua umuhimu wa kuendeleza utume wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Kristo, dhamana endelevu na pevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Wakristo wafundwe ili wafahamu Imani ambayo Kanisa linasadiki na kufundisha, Sakramenti zinazoadhikishwa na Mama Kanisa, Kanuni maadili yanayomwilishwa katika maisha ya watu kwa kujikita katika Amri za Mungu na Maisha ya Sala, ambayo kimsingi ni majadiliano kati ya mwamini na Muumba wake. Yote haya yalifahamika barabara, inakuwa rahisi kwa waamini kuweza kuyatolea ushuhuda kwa njia ya huduma makini katika sekta mbali mbali za maisha, kwani hiki kinakuwa ni kielelezo cha imani tendaji sanjari na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu.

Askofu mkuu Joseph Spiteri, Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe anabainisha kwamba, Uinjilishaji ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, anayetumwa kuwatangazia watu upendo na huruma ya Mungu. Kumbe, majiundo makini hayana budi kugusa undani wa mtu na kwamba, haya ni matunda ya umoja, ushirikiano na mshikamano wa Kikanisa. Waamini wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, wanatumwa kumshuhudia Kristo katika jamii wamoishi na kwa njia hii, wanaweza kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.