2015-05-05 07:46:00

Mashemasi wapya 14: Jengeni ari na moyo wa kimissionari katika huduma!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi, tarehe 2 Mei 2015 ametoa Daraja la Ushemasi wa mpito kwa majandokasisi 14 kutoka katika Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Mashemasi hawa ni kutoka Afrika na Asia. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati wa Familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amewataka Mashemasi wapya kutambua kwamba, wamewekwa wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa “visima na chemchemi ya furaha” hata pale watakapokutana na shida pamoja na vizingiti vya maisha na utume wao kwa Kanisa la Kristo.

Mashemasi wapya wameteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa na wanatumwa kwenda ulimwenguni kote ili kuwatangazia Watu Injili ya Matumaini. Wanapaswa kuendelea kushikamana na Kristo pamoja na Kanisa lake, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha kila wito. Yesu Kristo anajitambulisha kwa wafuasi wake kuwa ni Mzabibu wa kweli na kwamba Baba yake ndiye mkulima; matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha yanajikita katika muungano na mshikamano na Yesu Kristo. Tawi lisilo zaa matunda, litakiona che mtema kuni anasema Kardinali Filoni.

Mashemasi katika maisha yao, watambue kwamba, wao wamewekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake, changamoto na mwaliko wa kuiga na kufuata mfano wa Kristo aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni huduma ambayo inatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mashemasi wapya wanatoka: Tanzania,Uganda, Congo Brazzaville, Benin, Ghana, Nigeria, Cameroon, Korea na China. Haya ni maeneo ambayo watu wake wana kiu na hamu ya kutaka kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni na mioyoni mwao. Hapa mwaliko ni kukuza, kujenga na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Injili ya Furaha anasema kwamba, Kanisa linawahitaji Wainjilishaji wenye ari na moyo mkuu; wenye furaha na ujasiri; mashuhuda wa upendo wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.