2015-05-05 15:00:00

Licha ya mateso na madhulumu, jikiteni katika matumaini na mapendo


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki amehitimisha hija yake ya upendo na mshikamano wa kidugu na Wakristo huko Mashariki ya Kati, tarehe 5 Mei 2015 kwa kukutana na kungumza na viongozi wa Kanisa la Mashariki pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO. Katika hotuba yake, amewataka Wakristo huko Mashariki ya kati kujikita katika matumaini na mapendo, huku wakiendelea kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, mambo yanayojionesha katika Liturujia na Ibada mbali mbali zinazoadhimishwa na Mama Kanisa.

Katika ziara yake ya kikazi ameshuhudia mshikamano wa upendo na udugu unaojikita katika majadiliano ya kiekueme na kutekelezwa kwa moyo wa dhati na wafanyakazi wa ROACO, kwa ajili ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi; wote hawa wanastahili pongezi anasema Kardinali Sandri. Pia kuna haja ya kuepuka kushawishi cha kulalama pasi na sababu za msingi kwani Kanisa linajitahidi kutekeleza dhamana yake kadiri ya rasilimali iliyopo kwa kuzingatia pia kwamba, kuna mahitaji makubwa ya huduma.

Katika shida na magumu, katika mahangaiko na changamoto za maisha, hapo Wakristo wa Makanisa mbali mbali wanapaswa kushikamana kwa dhati na kuondoa kishawishi cha upendeleo au kwa baadhi ya waamini kujisikia kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine. Wakristo waendelee kuonesha upendo wao kwa Kristo kuwa waaminifu kwa Kristo mwenyewe pamoja na Kanisa lake.

Kardinali Sandri, Jumatatu, tarehe 4 Mei 2015 ameadhimisha Ibada ya Liturujia Takatifu katika Kanisa la Caldea huko Duhoq, nchini Iraq na kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha upendo na mshikamano kati ya Familia ya Mungu nchini Iraq unaosimikwa katika Agano ambalo Mwenyezi Mungu alifanya na watu wake. Hii ni changamoto ya kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wamekengeuka na kuanza kufanya vitendo vya mauaji, unajisi, ubakaji na uharibifu wa mazingira. Usaliti huu unafanywa hata na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuendelea kukaa kimya wakati watu wanauwawa kinyama na kuendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Lakini waamini wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi na maeno yake na utimilifu huu unajionesha kwa namna ya pekee kabisa na Yesu.

Ni matumaini ya Kardinali Sandri kwamba, ROACO litaendelea kuwa ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa Kristo na Kanisa lake, kwa kuwafariji na kuwahudumia wale wote waliopondeka moyo kwa divai ya upendo. Iko siku amani, itaweza kutawala katika maisha na mioyo ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.