2015-05-05 07:15:00

Iweni mashuhuda wa haki, amani na upatanisho, huru kutangaza Injili


Kanisa Katoliki nchini Congo halina budi kuendeleza mchakato wa upatanisho, haki na amani; kusaidia majiundo makini kwa waamini walei, ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu, daima wakisimama kidete kutangaza Injili ya Familia. Maaskofu wanapaswa kutekeleza dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa uhuru kamili na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano kati ya Makanisa mahalia, ili kuimarisha imani katika matendo.

Haya ni kati ya mambo msingi ambayo yametiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo, Jumatatu tarehe 4 Mei 2015 wakati huu wanapoendelea na hija yao ya kitume, inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Hiki ni kipindi cha kuimarisha umoja na mshikamano; ushuhuda na upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kanisa linaendelea kukua na kupanuka kwani kwa miaka ya hivi karibuni, kumeundwa majimbo mapya matatu, changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kusoma alama za nyakati na kujibu kiu na matamanio ya watu wengi ambao bado hawajasikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni mwao!

Baba Mtakatifu anawahamasisha Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanasaidia majiundo makini kwa waamini walei ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kwa njia hii wanaweza kuwa kweli ni vyombo vya ujenzi wa Familia ya Mungu inayojikita katika msingi wa umoja, haki na amani. Waamini walei wasindikizwe na kufundwa kadiri ya msingi wa Injili, ili kuishuhudia katika medani mbali mbali za maisha.

Kuhusiana na Sakramenti ya Ndoa, waamini hapa wanapaswa kufundishwa barabara sanjari na utamadunisho wa imani. Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu wa Congo kwa mchango wao wa dhati katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, kwani ni mchango ambao umegusa hali halisi ya Kanisa mahalia nchini Congo.

Mapadre ni wasaidizi wa kwanza wa Maaskofu, kumbe wanapaswa kuhudumiwa kikamilifu katika maisha na mchakato wa kutafuta utakatifu; mambo yanayohitaji majiundo makini ya awali na endelevu, ili waweze kujisadaka kikamilifu katika huduma kwa Familia ya Mungu nchini Congo. Wasaidiwe kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa uchaji na ibada; mahubiri yasaidie kurutubisha na kuimarisha imani ya waamini wao.

Maaskofu wathubutu kuwapeleka Mapadre wao kusoma hata nje ya nchi na kuhakikisha kwamba, wanawapatia mahitaji msingi, ili waweze kuhitimu mapema na kurejea tena nchini mwao, tayari kulitumikia Kanisa. Daima mafao ya Kanisa hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Kuna idadi kubwa ya miito ya Kipadre na kitawa, lakini miito hii haina budi kukuzwa, kuendelezwa kwa ajili ya mafao ya Kanisa, ili kupata watenda kazi jasiri, mahiri, wachapakazi, wema na watakatifu; wahudmu wa Injili wanaokumbatia Mashauri ya Injili. Familia ya Mungu ijihusishe kikamilifu katika majiundo ya Mapadre na Watawa.

Baba Mtakatifu anasema wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, kwa namna ya pekee anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa watawa wa mashirika mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa njia ya huduma makini: kiroho na kimwili kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Congo. Hawa ni mashuhuda wa Kristo: mtii, mseja na fukara. Mwaliko kwa Maaskofu ni kuendelea kushirikiana na kushikamana na watawa katika maisha na utume wao, ili kusaidia mchakato wa maendeleo ya Kanisa mahalia kwa kuchangia karama za Mashirika yao.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya Majimbo ambayo yana uhaba mkubwa rasilimali watu na fedha, hapa anapenda kuwaalika Maaskofu kujiwekea mikakati ya kuyategemeza majimbo yao sanjari na kushikamana kidugu, tayari kutangaza Injili ya Kristo pasi na vikwazo. Majimbo yashirikishane rasilimali mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Kanisa Barani Afrika halina budi kuwa ni la kimissionari zaidi.

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu kujenga na kuimarisha umoja wa Kikanisa kwa kuunganisha sauti zao, ili kweli ziwe ni sauti za kinabii; kwa kuonesha umoja katika tofauti; kwa kusimama kidete kutafuta mafao ya wengi pamoja na yale ya Kanisa. Maaskofu washikamane ili kukabiliana na changamoto za shughuli za kichungaji nchini mwao, tayari kujikita katika azma ya Uinjilishaji unaowataka kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kuendelea kumhudumia mtu mzima kiroho na kimwili: katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, bila kuwasahau wahamiaji na wageni kutoka katika nchi jirani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kanisa halina budi kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho nchini Congo kwa kutambua kwamba, machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kunako miaka ya 1990, yameacha madonda makubwa ya utengano; hapa Kanisa linatumwa kuwapatanisha watu, ili kujenga umoja na udugu unaosimikwa katika msamaha na mshikamano; viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa kweli ni mfano wa kuigwa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kuzinduliwa kwa Madhabahu ya Huruma ya Mungu Jimboni Dolisie, mahali ambapo kwa sasa panatumika kama sehemu ya hija, mafungo na mikutano ya maisha ya kiroho; pataendelea kuwa ni mahali pa kuimarisha imani na kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Mwishoni, anawatakia kheri na baraka Watu wa Mungu wanaoendelea kufanya hija ya maisha nchini Congo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.