2015-05-05 09:27:00

Expo Milano 2015: Watu wana njaa na kiu ya kiroho na kimwili!


Onesho la chakula kimataifa la Expo Milano 2015, limefunguliwa kwa hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe Mosi, Mei, 2015 kwa kugusia kuhusu kashfa ya baa la njaa na umuhimu wa Jumuiya ya kimataifa kushikamana katika mapambano dhidi ya njaa na utapiamlo wa kutisha duniani, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Onesho hili linazihusisha nchi 145. Rais Sergio Mattarella anasema, onesho hili liwe ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe katika kuilisha dunia, kwani chakula ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya watu. Kwa Italia hii ni fursa ya kuwekeza zaidi katika mapambano dhdi ya baa la njaa duniani.

Kardinali Giafranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anabainisha kwamba, mwanadamu anakabiliwa na njaa ya maisha ya kiroho na kimwili, ndiyo maana, Vatican imekuwa ikishiriki katika maonesho mbali mbali ya kimataifa, tangu kunako mwaka 1851, wakati wa uongozi wa Papa Pio IX. Kanisa lilishiriki katika onesho la kazi na mazao ya viwanda. Kunako mwaka 1964, Vatican ikashiriki pia kwa onesho la picha maalum za Michelangelo, ambazo kwa mara ya kwanza ziliweza kutolewa kwenye jumba la makumbusho la Vatican. Wakati huu, Vatican inashiriki katika Onesho la chakula la Milano kwa kuchangia tafakari kuhusu umuhimu wa chakula cha kiroho na kimwili katika maisha ya mwanadamu!

Kardinali Ravasi anabainisha kwamba, Kanisa linapenda kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe katika kupambana na baa la njaa pamoja na utapiamlo w akutisha, mambo ambayo kwa sasa ni kashfa kubwa kwa karne ya ishirini na moja. Hii inatokana na ukweli kwamba, dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya watu wote.

Banda la Vatican linaongozwa na vifungu vya Maandiko Matakatifu vinavyonesha kwamba, mtu hawezi kuishi kwa mkate peke yake, na kwamba, anahitaji kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumkirimia chakula cha kila siku. Kwa bahati mbaya, bado kuna umati mkubwa watu wanaokufa kwa baa la njaa duniani, wakati ambapo kuna chakula cha kutosha! Watu wana njaa ya chakula cha kimwili pamoja na chakula cha kiroho, ndiyo maana kuna tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, chakula kinachoshibisha njaa ya maisha ya kiroho, tayari kujisadaka kwa kujenga madaraja ya mshikamano, umoja na upendo wa kidugu.

Dhana ya chakula anasema Kardinali Ravasi inafumbata pia masuala msingi katika maisha ya mwanadamu: kiafya, kijamii, kielimu na hata kiuchumi. Shirikisho la Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika onesho hili linajikita katika baa la njaa kwa kuonesha madhara ya njaa duniani pamoja na mbinu mkakati zinazoweza kutumiwa kwa ajili ya kupambana na njaa duniani.

Hospitali ya Bambino Gesù, inaangalia masuala ya lishe bora na madhara yanayotokana na lishe duni katika afya ya mwanadamu. Madhara ya wasichana wanaotaka kuwa walimbwende, kwa kujinyima chakula, kiasi cha kubaki kama mifupa! Waingereza wanasema, eti wanabaki ”Skeleton tupu”. Wanapenda kuonesha umuhimu wa akina mama wazazi kuwaonyonyesha watoto wao na masuala ya tiba katika mambo ya chakula.

Baraza la Kipapa la utamaduni hapo tarehe 11 Juni 2015 litafanya tafakari ya kina kuhusu baa la njaa duniani; mabadiliko ya tabianchi na athari zake; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Banda la Vatican limeweka kisonzo kwa ajili ya kuchangia mapambano dhidi ya baa la njaa, dhamana inayotekelezwa na Kanisa kama sehemu ya dhamana na maisha yake. Watu wanaotembelea onesho la chakula la Expo Milano 2015, wanaalikwa kuchangia kwa ajili ya kuwezesha huduma zinazotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, Vatican inapenda kushiriki, si tu kwa maneno, bali kwa njia ya mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.