2015-05-04 08:21:00

Wakristo Mashariki ya Kati: Changamoto ya kimataifa na Kanisa!


Umuhimu wa uwepo endelevu wa Wakristo huko Mashariki ya Kati; changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakomesha mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo, sanjari na kusitisha wimbi kubwa la Wakristo wanaokimbia kutoka Mashariki ya Kati na kwamba, Kanisa lina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Haya ni kati ya mambo makuu ambayo yametiliwa mkazo na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati akichangia mada kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu hatuma ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, uliokuwa unafanyika mjini Bari, Kusini mwa Italia.

Askofu mkuu Gallagher anabainisha kwamba, Kanisa limekuwa likifuatilia kwa karibu zaidi hali ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati kwa kutumia njia za kidiplomasia na katika uwanja wa Jumuiya ya Kimataifa; kwa kushirikiana na viongozi wakuu wa Makanisa na mara nyingi Baba Mtakatifu amegusia changamoto hii katika mikutano, hotuba na tafakari zake, kiasi hata cha kuwaandikia barua Wakristo huko Mashariki ya Kati, ili kuwatia moyo kusonga mbele kwa imani na matumaini, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo. Zote hizi ni jitihada za ujenzi wa mshikamano wa upendo na udugu.

Askofu mkuu Gallagher anasema kwamba, Wakristo Mashariki ya Kati wanayo haki na wajibu wa kuendelea kukaa katika eneo hili na kwamba, wao ni sehemu ya utamaduni na mapokeo ya wananchi wanaoishi eneo la Mashariki ya Kati. Uwepo wao ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa sanjari na ustawi na maendeleo endelevu. Wakristo hawa ni sawa na chachu ya maendeleo, demokrasia ya kweli na haki msingi za binadamu na kwamba, wanao wito maalum wanaopaswa kuuendeleza kwa ajili ya mafao ya wengi.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulivalia njuga ili kusitisha tatizo la mauaji, nyanyaso na dhuluma ambazo zimepelekea wimbi kubwa la Wakristo kukimbia huko Mashariki ya Kati. Kanisa lingependa kuona usalama wa watu na mali zao. Machafuko ya kisiasa ambayo yamedumu kwa takribani miaka minne sasa yamepelekea adha kubwa kwa wananchi huko Mashariki ya Kati. Kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji msaada wa dharura. Matatizo na changamoto zote hizi zinaweza kufumbuliwa ikiwa kama uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu vitazingatiwa pamoja na kuheshimu dhamiri za watu.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kukomesha vita ili kutoa nafasi kwa wakimbizi na wahamiaji kurejea tena katika makazi na maeneo yao, tayari kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu, kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upatanisho, majadiliano na maridhiano. Amani ya kweli ni cheche za matumaini na maendeleo huko Mashariki ya Kati.

Jumuiya ya Kimataifa ijiwekee mikakati ya kuzuia mauaji ya kimbari yasijirudie tena huko Mashariki ya kati kwa kupambana kikamilifu na vitendo vya kigaidi na watu wanaofadhili ugaidi katika ngazi mbali mbali. Jumuiya ya Kimataifa iwe makini na mafundisho yanayotolewa kwenye nyumba za Ibada na kwenye taasisi za elimu, ili kudhibiti wimbi la uwepo wa misimamo mikali ya kidini, inayohatarisha amani, ustawi na mfungamano wa kijamii. Mahusiano kati ya dini na serikali ni uwanja mwingine unaopaswa kufanyiwa kazi, ili kudumisha haki na uhuru wa kuabudu.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican anaendelea kuchambua mchango wa Kanisa huki Mashariki ya kati: Mosi, Kanisa limeendelea kuhamasisha mshikamano wa upendo na udugu kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati. Wakristo wameendelea kuhimizwa kubaki katika maeneo yao, kwani wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu. Kanisa haina budi kuendelea kuwekeza kwenye majiundo makini kwa waamini walei, ili waweze kushiriki barabara katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

Askofu mkuu Gallagher anasema, licha ya Wakristo kutoka Mashariki ya Kati kuendelea kupungua, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta fursa za ajira huko Mashariki ya Kati. Kumbe, mauaji, mateso na nyanyaso wanazokabiliana nazo ni changamoto ya kujikita katika mchakato wa Uekumene wa damu, kama kiini cha umoja na mshikamano wa Wakristo, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao.

Mashariki ya Kati inakabiliwa na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi katika ngazi ya kisiasa, kidiplomasia na kichungaji, kumbe, Wakristo wanakumbushwa kwamba, Yesu ni Bwana wa historia ya mwanadamu, huyo ndiye ambaye Kanisa linamkabidhi hatima ya Wakristo huko Mashariki ya kati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.