2015-05-04 11:11:00

Tamasha la Vijana Kitaifa Uswiss: Kipindi cha Sala, Tafakari na Muziki


Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss kuanzia tarehe Mei Mosi, hadi tarehe 3 Mei, 2015 kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, limeendesha Siku ya Vijana Kitaifa, iliyowakusanya vijana kutoka sehemu mbali mbali kwa ajili ya kusali, kutafakari na kufurahia zawadi ya maisha kwa njia ya tamasha la muziki. Siku ya vijana kitaifa imeongozwa na kauli mbiu “Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu”, mada ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, itakayofanyika kunako mwaka 2016 Jimbo kuu la Cracovia, Poland.

Siku ya vijana kitaifa nchini Uswiss limewashirikisha vijana wa kizazi kipya kuanzia umri wa miaka 16 hadi miaka 35, kwa siku tatu, wasemali, wamesikiliza, wamecheza na kukutana na Maaskofu wao. Imekuwa ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwaonjesha vijana upendo na mshikamano unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wamugundua ndani mwao, ujana wa Kanisa unaofumbatwa katika maisha, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Familia nyingi zimetoa nafasi kwa vijana kupata malazi na chakula cha asubuhi, jambo ambalo limejenga mshikamano wa upendo.

Vijana wa kizazi kipya, wamejirushwa kwa tamasha la muziki kutoka kwa wanamuzi vijana mashuhuri nchini Uswiss, lakini kwa wakati huu, muziki wao umejikita katika Maandiko Matakatifu. Vijana wamekutana na walimbwende waliokuwa wanavuma enzi zao katika mashindano ya urembo duniani, lakini leo hii ni watu wa familia, wenye heshima na dhamana katika maishaya ndoa na familia.

Vijana wamekumbushwa kwamba, ujana ni mali, lakini fainali ni uzeeni, kumbe wanapaswa kuutumia vyema ujana wao kwa kujikita katika mambo msingi. Huu ni ushuhuda ambao umetolewa na vijana waliokuwa wamekubuhu kwa kushiriki katika magenge ya wizi wa magari Barani Ulaya, lakini, wakatubu na kuongoka, leo hii ni watu wema, fedha, mali na fahari ya dunia ni mambo ya mpito; jambo la msingi ni kukuza na kudumisha utu na heshima kama binadamu, kwani mengine yote yanapita.

Imekuwa ni fursa kwa Maaskofu Katoliki kutoka Uswiss kuweza kuwasikiliza vijana kwa makini, kwa kuandamana nao katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu; tafakari ya Neno la Mungu kama dira na mwongozo wa maisha; kwa Katekesi makini, ili waweze kutambua mafundisho tanzu ya Kanisa, tayari kuyatolea ushuhuda katika maisha yao ya ujana, kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Jumapili tarehe 3 Mei 2015, vijana wamehitimisha Kongamano la kitaifa kwa kubadilishana mawazo, changamoto na matumaini, tayari kutweka hadi kilindini kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.