2015-05-04 07:48:00

Onesheni moyo wa toba na wongofu wa ndani: shuhudieni imani tendaji


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 3 Mei 2014 ametembelea na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika Parokia ya Regina Pacis, iliyoko Ostia nje kidogo ya mji wa Roma. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu amepita na kuwasalimia Watawa wa Shirika la Mtakatifu Charles de Foucald, wanaotekeleza maisha na utume wao kwa moyo wa Injili, katika ukimya, sadaka, sala na tafakari ya Neno la Mungu. Baba Mtakatifu amekutana na wagonjwa, wazee, vijana na familia za watoto waliobatizwa katika kipindi cha mwaka uliopita.

Baba Mtakatifu amewaungamisha waamini wanne, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, changamoto kwa waamini kuithamini Sakramenti ya Upatanisho katika hija ya maisha yao ya kiroho. Wakati wa mahubiri, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa waamini kushikamana na Yesu, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Kushikamana na Yesu kunafumbatwa katika maisha ya sala, huduma makini kwa wagonjwa na maskini pamoja na kukimbilia huruma na upendo wake unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho. Sala haitaweza kuzaa matunda, ikiwa kama mwamini hajaungana kikamilifu na Yesu.Waamini wakikaa ndani ya Yes una kuyashika maneno yake, wataweza kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na jamii inayowazunguka.

Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na vijana Parokiani hapo amewajibu maswali waliyomuuliza kuhusu jinsi gani wanavyoweza kuonesha furaha katika huduma sanjari na kushuhudia Injili. Baba Mtakatifu anawataka vijana kupanga na kuchagua mambo msingi katika maisha yatakayowawezesha kupata furaha ya kweli; pale wanapoanguka, wajitahidi kusimama na kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa.

Jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kutambua kwamba, furaha ya kweli ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu, inayomwezesha mwamini kuwa na mwelekeo chanya katika maisha. Hata katika mahangaiko yao ya ndani, wawe na uvumilivu unaotunza heshima na utu wao na kuondokana na kishawishi cha kutumbukia katika ubinafsi.

Baba Mtakatifu Francisko amepata fursa pia ya kukutana na kusalimiana na wazee pamoja wagonjwa kabla ya kuanza Ibada ya Misa Takatifu. Wazee wanahifadhi ndani mwao hekima, uzoefu na maarifa ya maisha, ni watu wanaoweza kuvumilia mateso na mahangaiko kwa imani na matumaini. Wazee ni maktaba ya familia na jamii inayowazunguka; wagonjwa ni kundi linaloendelea kubeba Msalaba pamoja na Yesu. Hii ni changamoto kwa jamii kuhakikisha kwamba, inawahudumia wazee na wagonjwa. Amewaomba kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka yao ya kila siku.

Kabla ya kuondoka na kurejea tena mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na umati mkubwa uliokuwa umebaki nje, kwa kukosa nafasi wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Anasema, anatambua jinsi ambavyo ni vigumu kufuatilia Ibada iliyokuwa inafanyika ndani ya Kanisa. Anawashukuru kwa mapokezi na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija ya kichungaji Parokiani hapo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.