2015-05-04 10:57:00

Msanii Dante Aligheri: Nabii wa matumaini, uhuru na mageuzi ya kweli!


Nchi ya Italia inafanya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 750 tangu alipozaliwa Msanii maarufu Dante Aligheri, tukio ambalo limeshuhudiwa na Rais Sergio Mattarella, viongozi wakuu wa Serikali ya Italia pamoja na wasanii maarufu kwenye Ukumbi wa Madama, Roma. Katika tukio hili, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa ajili ya kumbu kumbu hii, ambayo ni urithi na utajiri mkubwa ulioachwa na Msanii huyu ambaye anawasaidia watu kupitia katika njia ya ufahamu, ukweli wa mtu kugundua undani wa maisha yake na maana halisi ya mambo yanayopita akili na ufahamu wa binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kazi za msanii Dante Aligheri zimekuwa zikipongezwa na watangulizi wake kama Benedikto wa kumi na tano kutokana na mchango wake katika majiundo makini ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu; Mwenyeheri Paulo VI, wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican alimsifia na kumpongeza Dante kutokana na mchango wake katika kurithisha imani ya Kanisa inayomletea mwamini mabadiliko ya kweli. Hii inatokana na ukweli kwamba, maudhui ya msanii huyu yanajikita katika kanuni maadili, hekima; anaonesha madhara ya dhambi na umuhimu wa kuchuchumilia utakatifu na maisha yanayojikita katika furaha ya kweli.

Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, wamemtaka Dante kuwa ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushairi na kwamba, hata Papa Francisko katika Waraka wake wa kichungaji Mwanga wa Imani, Lumen Fidei, ametumia utajiri wa alama na vielelezo vilivyotolewa na Dante ni mwanga unaofafanua imani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu utakaozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015, ili fursa ya kufufua na kuendeleza mchango uliotolewa na Dante, sanjari na maandalizi ya kumbu kumbu ya miaka mia saba tangu alipofariki dunia, hapo mwaka 2021.

Kazi ya Dante isomwe kwama hija ya maisha ya binadamu kwa kuondokana na mambo yanayowafanya kuwa wakatili na badala yake kukumbatia: maridhiano, amani na furaha, kielelezo cha kweli cha ubinadamu. Dante ni nabii wa matumaini, uhuru na mageuzi ya kweli; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.