2015-05-04 07:11:00

Mkristo mwema ni chombo cha mafao kwa jirani na jamii inayomzunguka


Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, saa yake ilipokuwa imewadia, Yesu alipenda kuwaachia urithi wafuasi wake, ili waweze kuendelea kushikamana pamoja naye, ili hatimaye, waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwani nje yake, wangenyauka na kutupwa. Yesu akajifananisha na Mzabibu na kwamba, wafuasi wake wote ni matawi, ili waweze kuzaa matunda ajaa hawana budi kushikamana na Yesu. Kwa kushikamana na Yesu, wanafunzi wake, wanatambua uwepo wake endelevu na kuonjeshwa upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Jambo la msingi ni kushikamana na Yesu.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala la Malkia wa mbingu, Jumapili tarehe 3 Mei 2015, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uliokuwa umesheheni watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wamepokea zawadi ya maisha mapya, changamoto ni kuendelea kushikamana na Yesu kwa kuwa waaminifu kwa ahadi za Ubatizo. Huu ni mwaliko wa kudumisha urafiki kwa njia ya sala za kila siku, kusoma, kusikiliza na kulitafakari Neno la Mungu katika hali ya unyenyekevu. Lakini zaidi ni kushiriki maisha ya Kisakramenti, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, ikiwa kama mwamini ameungana barabara na Yesu, atawezeshwa kupokea karama za  Roho Mtakatifu ambazo ni: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi na matokeo yake ni mafao kwa jirani na jamii nzima. Huu ndio utambulisho wa Mkristo unaojidhihirisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kwani mti unatambulikana kutokana na matunda yake. Neema ya Roho Mtakatifu inamwezesha mwamini kufanya mabadiliko katika maisha yake; kwa njia hii, maisha ya Kristo yanakuwa ni maisha ya mwamini, kwa kufikiri, kuona na kutenda kama Yesu mwenyewe.

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia hii, waamini wanaweza kuonesha upendo kwa jirani kwa kuanzia na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama vile Yesu alivyowapenda mwenyewe kwa moyo wake wote, na hivyo dunia itaweza kukirimiwa matunda ya wema, upendo na amani. Waamini wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanazaa matunda ambayo ni kielelezo cha umoja na mshikamano na Yesu Kristo; kwa kushuhudia imani tendaji, inayomwilishwa katika mawazo na maisha, kila mtu kadiri ya wito wake, kwani kwa pamoja wanashiriki utume wa Ukombozi ulioanzishwa na Yesu Kristo.

Mara baada ya sala ya Malkia wa mbingu, Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wanachama wa Chama cha Metèr, katika maadhimisho ya Siku ya watoto wahanga wa nyanyaso. Anawashukuru kwa kusimama kidete kutetea maisha ya watoto dhidi ya uhalifu huu. Watu wote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuwalinda na kuwatetea watu, hususan watoto wadogo.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Luigi Bordino wa Shirika la Ndugu wa Mtakatifu Yosefu Benedetto Cottolengo, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri kwenye Jimbo kuu la Torino, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Angelo Amato. Ni mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya wagonjwa na wote waliokuwa wanateseka; akajitosa kimasomaso kuwasaidia maskini, kwa kuwapatia tiba na kusafisha madonda yao. Kanisa lina mshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya mfuasi wake mnyenyekevu na mkarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.