2015-05-04 09:26:00

Kanisa Katoliki Congo: Changamoto na vipaumbele vya kichungaji


Umwilishaji wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, majiundo makini ya Wakleri na walei; haki, amani na upatanisho ni kati ya changamoto na vipaumbele vya shughuli za kichungaji kwa Kanisa nchini Congo, Brazzaville. Kanisa linaendelea kukua na kuchanua kama mtende wa Lebanon katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Kanisa Katoliki nchini Congo linaundwa na Majimbo tisa. Kuna ongezeko la miito mitakatifu ya Upadre na Utawa, lakini bado mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Ndiyo maana Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linaendelea kuwahamasisha waamini kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu, ili Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi, wema, watakatifu, wanyofu na wachapakazi, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Idadi ya Wakristo inaendelea kuongezeka maradufu, changamoto kubwa iliyoko mbele ya Kanisa ni kuhakikisha kwamba, wanawezeshwa kuyafahamu mafundisho tanzu ya Kanisa, tunu msingi za maisha ya Kikristo  na kiutu, tayari kuzitolea ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji. Hapa kuna haja ya kujikita katika maisha ya Sakramenti ya ndoa na kuondokana na uchumba sugu, ambao ni changamoto kubwa kwa waamini nchini Congo.

Baraza la Maaskofu katika mkutano wake wa hivi karibuni, limeandika baraua ya kichungaji inayoonesha mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi, ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza Injili ya Familia na Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo. Kama sehemu ya mkakati wa shughuli za kichungaji, Maaskofu wanaendelea kuwekeza katika majiundo makini ya waamini walei, ili kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda makini, wenye mvuto na mguso katika medani mbali mbali za maisha.

Haya ni majiundo ya awali na endelevu yaliyokuwa yametolewa mkazo na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI wakati Baraza la Maaskofu Katoliki Congo lilipofanya hija ya kitume mjini Vatican kunako mwaka 2007. Waamini wanapaswa pia kufundishwa, Maandiko Matakatifu, Katekisimu ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa, nyenzo muhimu katika kuyatakatifuza malimwengu. Lengo ni kukoleza utakatifu wa maisha, umoja, upendo na mshikamano wa Familia ya Mungu nchini Congo dhidi ya ukabila na kinzani za kijamii.

Baraza la Maaskofu katoliki Congo linabainisha kwamba, kati ya changamoto zinazofanyiwa kazi ni pamoja na: haki, amani na upatanisho; mambo ambayo kwa sasa yanachangiwa na migawanyiko ya kisiasa, iliyopelekea vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kanisa linaendelea kuifanyia kazi changamoto hii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Congo.

Kwa namna ya pekee, Kanisa linamkumbuka na kumwombea Kardinali E’mile Biayenda, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Brazzaville aliyeuuwawa kikatili kunako mwaka 1977. Imekwishagota miaka 38 tangu mauaji ya chuki ya imani “in odium fidei” yalipotokea. Damu yake isiyokuwa na hatia, iwe ni mbegu ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Ikumbukwe kwamba, familia ni kitalu na shule ya kwanza ya haki, amani, upatanisho, mshikamano na udugu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linasema, kuna haja kwa Serikali na wadau mbali mbali kuwekeza katika huduma makini za kijamii hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya watu kwa kupambana na ujinga, umaskini ma maradhi, maadui wakuu wa nchi. Kuna haja ya kufanya maboresho makubwa katika elimu, ili wanafunzi waweze kupata elimu bora zaidi, kuliko hali livyo kwa sasa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linaendelea kuwekeza katika mchakato wa majiundo makini kwa Wakleri na Watawa, ili kujenga na kuimarisha Kanisa ambalo linajikita katika mwelekeo wa kimissionari, tayari kutoka ili kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha, Amani na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Ushuhuda maisha ya Kipadre na kitawa yanayosimiwa katika tasaufi na utume ni mambo yanayopewa kipaumbele kwa sasa.

Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanaendelea kuhamasishwa ilikuhakikisha kwamba, yanatoa majiundo makini na endelevu kwa watawa wao, ili kweli Kanisa liweze kuwapata watenda kazi hodari, watakatifu na wachamungu tayari kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Kwa ufupi, hizi ndizo changamoto na vipaumbele vinavyotolewa na Kanisa Katoliki nchini Congo, Brazzaville katika maisha na untume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.