2015-05-04 08:13:00

Kamanda anapaswa kuonesha ujasiri, unyenyekevu na umoja katika huduma


Kamanda Christoph Graf wa Kikosi cha Ulinzi cha Waswiss maarufu kama Swiss Guards, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe Mosi, Mei 2015 ameongoza gwaride la heshima kwa ajili ya kuzindua bendera mpya ya Kikosi hiki, sherehe ambazo zimehudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Vatican.

Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, sherehe hizi zilitanguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyooongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ambaye pia alibariki bendera mpya. Baadaye likafuatia gwaride la heshima. Kanali Christoph Graf ametoa hotuba ya shukrani na utii kwa Baba Mtakatifu Francisko, kama “Kamanda mkuu” wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amemtakia kheri, baraka na ufanisi Kamanda Graf anapoanza utume wake. Kama kiongozi mkuu anapaswa kuhakikisha kwamba, anajikita katika ujenzi wa umoja, upendo na udugu; mambo yanayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu. Aoneshe fadhila ya kibaba kwa wanajeshi ambao wamedhaminishwa kwake; awe ni mtu wa sala, ili aweze kupandikiza mbegu ya umoja na upendo miongoni mwa wanajeshi wake.

Kama kiongozi wa kijeshi, anapaswa kuwa ni mtu mwenye ujasiri na unyenyekevu, kama motto yake inavyoonesha “Mut und Demut”. Kuongoza kadiri ya mafundisho ya Kanisa ni kuinjilisha. Baba Mtakatifu baada ya kutoa nasaha hizi chache, amewapatia baraka zake za kitume, wanajeshi, familia na wageni waliokuwa wamekusanyika kushuhudia tulio hili la kihistoria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.