2015-05-04 09:44:00

Jubilei ya Huruma ya Mungu: Yesu Kristo ni kioo cha Huruma ya Mungu


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Karibu katika kipindi hiki ambapo kwa wakati huu tunaipitia barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Fransisko, maalumu katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Inaitwaje? Misericordiae vultus, yaani Uso wa Huruma. Mungu ni mwema sana kwetu nyakati zote, daima anatuelekezea huruma yake kuu katika mazingira mbalimbali na kwa namna mbalimbali.

Katika kipindi kilichopita tulialikwa sote kuimwilisha huruma hiyo ya Mungu tunayoonjeshwa sisi wenyewe kwa njia ya kuiishi na kuwashirikisha wenzetu pia. Na kioo-mfano cha huruma ya Mungu ni Kristo mwenyewe, anayetuita katika Neno lake kuenenda kwa huruma kama baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma. Tunapoitafakari, kuishukuru na kuitangaza huruma kuu ya Mungu, tuendelee kumwomba tukisema, “Bwana utuekelezee uso wako mpole, nasi tutakuwa salama”.

Katika kipindi hiki Mpendwa msikilizaji, kutoka katika Hazina yetu ya Misericordiae Vultus, uso wa huruma, tunaendelea nasi kutafakari wajibu wetu wa kibinadamu wa kusoma mioyo ya watu na maisha ya watu, na kisha kuona namna sahihi ya kuwajibika kuelekeza huruma ya upendo kama Kristo mwenyewe alivyofanya, wakati ule alipowaona makutano wamechoka, wametawanyika kama kondoo wasio na mchungaji...aliwahurumia, akajibu vilio vya mioyo yao.

Na katika hili tulielekezwa kwamba, tukwepe kabisa kishawishi cha kujivua fahamu. Tusijifanye hatuoni au hatusikii au hatuelewi chochote. Fumbua macho – tazama, zibua masikio – sikiliza, fumbua akili – fikiri upate kujua ni namna gani unaweza walao ukamwonjesha huruma ya Mungu huyo aliye karibu yako hapo kwanza. Usiwaze kwenda mbali sana. Anzia hapohapo ulipo, katika familia yako, anzia hapo hapo kazini kwako kwa wafanyakazi wenzako, anza na huyo maskini mhitaji unaemwona hapo mbele zako.

Kila mmoja wetu anaweza kuwaonjesha watu huruma, iwapo tu anataka. Nyezo tumepewa na Mungu mwenyewe. Kugusa vilio vya watu, yaweza kuwa kwa njia ya sala, mawazo mema yanayomwilika katika ushauri mwema, ushauri wenye kujenga, ushauri wenye kuinua, ushauri wenye kufariji; na pia kwa njia ya matendo ya upendo. Katika hayo, kila binadamu anaweza.

Na tuone kuwa ni wajibu wetu sisi sote kutoa na kupokea huruma. Hayupo aliyezalikwa kwa ajili ya kuhurumiwa tu, hapana! Na hayupo ambaye kazi yake ni kuhurumia tu, kana kwamba yeye hahitaji chochote kutoka kwa yoyote. Sote tunahimizwa kupokea na kutoka huruma ya Mungu. Ni kwa njia hiyo mimi na wewe tunakuwa ni wajumbe wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anaendelea kumwonesha Kristo kama kioo kweli cha huruma ya Mungu. Anadhihirisha hilo katika matukio mbalimbali ya kugusa matatizo ya watu. Huruma ya Mungu si jambo la kusemwasemwa tu au kuimbwa imbwa, ni jambo la kuishi katika matendo yanayoonekana. Na daima Kristo ameonesha mfano wa kugusa kwa huruma. Huruma katika matendo. Mfano mwingine ni huu:-

Pale alipoingia mji wa Naim na akakuta watu wabeba jeneza wanakwenda kumzika mwana wa pekee wa mjane mmoja. Alimhurumia huyu mama aliyekuwa katika uchungu mkuu. Kwanza tayari alikuwa na uchungu wa kuwa mjane, halafu mjane mwenye mtoto mmoja, na huyo mtoto moja naye ndiyo anapelekwa kuzikwa. Hivi uchungu wa huyu mama mjane ulikuwa mwingi kutosha kutokana na mlundikano wa matatizo. Kristo alimhurumia, akamfufua yule kijana mfu (rej. Lk 7:15).

Na Kristo daima baada ya kutuonjesha huruma yake, anatupatia utume maalumu, wa kuipelekeka huruma hiyo kwa wenzetu. Siku ile, baada ya kumwondolea mapepo yule mtu katika nchi ya Wagenesareti, alimpa utume akasema “nenda nyumbani kwa ndugu zako, ukawaambie jinsi gani Bwana alivyokutendea, na namna alivyokuonesha huruma yake” (Mk 5:19).

Katika maisha yetu, mara nyingi wengi wetu tunaogopa au tunaona aibu kuishuhudia huruma ya Mungu. Watu wengi ili kuiishi huruma ya Mungu, wanahitaji ushuhuda wa wale ambao tayari wamekwisha kuonja huruma ya Mungu. Watu wengi wanateseka, wanaendelea kujitwisha karai la moto sana kwa sababu sisi hatujatoa ushuhuda wa huruma ya Mungu. Ukiinuliwa kwa huruma ya Mungu, usisahau kuwainua na wenzako, ili tufurahi wote na kama sio wote basi wengi.

Mpendwa msikilizaji, tukiangaziwa na barua hii ya kitume Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, tunaona kwamba, ili kuwa kweli wajumbe wa huruma ya Mungu, ni vema kupiga vita kabisa vilema vya wivu, ubinafsi, kijicho, kujikwenza, maringo, ubaridi na uzembe, na mambo yanayofanana na kama hayo. Kwani vilema hivyo ndiyo vinatuziba macho ya roho na mwili ili tusiwafikie binadamu wenzetu.

Asante kwa kuisikiliza Radio Vatican, tusisahau kuitumia ile dawa kiboko ya njia aliyotupatia Baba Mtakatifu Fransisko yaani, kusali rozali ya huruma ya Mungu, ili Mungu mwenye huruma atuhurumie sisi na dunia nzima.

Kutoka katika studio za radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.