2015-05-04 10:18:00

Jengeni na kuboresha maisha yenu kwa njia ya urafiki na Yesu!


Urafiki kati ya Kikosi cha Ulinzi Cha Kipapa kutoka Uswiss, maarufu kama Swiss Guards na Khalifa wa Mtakatifu Petro, unabubujika kutoka katika upendo wa Kristo aliyejisadaka kwa ajili ya binadamu ili kumkirimia maisha tele. Katika historia ya Kanisa, kuna watu wengi ambao wamejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kama ilivyokuwa kwa wanajeshi kutoka Uswiss, waliojitosa kumlinda Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha kumfuasa Kristo.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, siku ya Jumatatu tarehe 4 Mei 2015 alipokutana na wanajeshi wa Kikosi cha Kipapa kutoka Uswiss pamoja na ndugu, jamaa na viongozi mbali mbali wa Vatican, wakati wanajeshi hawa walipokuwa wanajiandaa wanakula kiapo cha utii, Jumatano tarehe 6 Mei 2015 tayari kumfuasa Yesu Kristo Mfalme, ili kujenga na kuimarisha ufalme wake, kwa kushirikiana na binadamu. Dhamana hii inahitaji watu wenye msimamo na ujasiri katika maisha, ili kushikamana na Yesu kikamilifu. Ni mwaliko wa kulinda na kukesha, ili hatimaye, waweze kushiriki katika ushindi dhidi ya Shetani.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ndiye Mfalme wa kweli na rafiki zake wanamfuasa na kwamba, askari wa Yesu anashiriki pia katika maisha yake, changamoto kwa wanajeshi kutoka Uswiss kushiriki katika dhamana na utume huu kwa kuambatana na Yesu. Wawe makini kujifunza siku kwa siku kujisikia na Kristo pamoja na Kanisa lake; kwa kumfuasa na kulipenda Kanisa; kwa kushuhudia imani ya kweli.

Maisha haya yanaweza kuboreshwa kwa njia ya ushiriki katika Sakramenti za Kanisa; maisha ya sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Wakuze ndani mwao Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, wagonjwa na wale wanaotafuta neno la faraja. Daima wanapokutana na mahujaji na wageni wanaofika mjini Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia, basi wawaonjeshe: wema, ukarimu na upendo unaobubujika kutoka kwenye urafiki na Kristo. Wanajeshi hawa ni utambulisho wa Vatican.

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, kazi na huduma yao ni pevu kwani daima kunapokuwepo na hitaji, wao wako tayari kabisa kujitosa bila ya kujibakiza. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa huduma hii tete wanayoitekeleza kwa ajili ya Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.