2015-05-02 16:22:00

Mwenyeheri Luigi wa Consolata alikita maisha yake katika huduma makini


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi tarehe 2 Mei 2015 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Fra Luigi Bordino, aliyeishi kati ya mwaka 1922 hadi mwaka 1977 kuwa Mwenyeheri. Luigi wa Consolata kama alivyojulikana na wengi alikuwa ni mtawa aliyejipambanua kwa huduma makini kwa wagonjwa na kati ya watu waliokuwa wanajitolea kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu; aliowanjesha wagonjwa na maskini chemchemi ya Injili ya Furaha.

Kabla ya kuacha yote na kujiunga na maisha ya kitawa, Luigi wa Consolata alikuwa ni mkulima bora wa zabibu huko Cuneo, alikuwa ni mchezaji mzuri wa mpira; wengi walimwona kuwa kweli ni kijana mwema na mtakatifu, wakavutiwa na ushuhuda wa maisha yake. Alipenda kuwafariji wagonjwa na maskini, kwani ndani mwao aliiona ile sura ya Kristo mteswa. Alikuwa ni kijana mwenye Ibada kwa Bikira Maria na daima alipenda kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili.

Luigi wa Consolata alijibidisha kuboresha maisha yake ya kiroho kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na mahusiano mema na jirani zake. Mazingira yote haya yakamjengea uthabiti wa moyo na ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, yaliyokuwa yanamwilishwa katika huduma ya huruma na mapendo. Ni kijana aliyeshiriki katika Vita kuu ya Pili ya Dunia, akashuhudia mateso na mahangaiko ya watu kutokana na madhara ya vita. Akaonjeshwa suluba ya kutekwa nyara na kupelekwa uhamishoni, huko Siberia na kufanikiwa kurejea tena Italia mara baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Baada ya kusoma alama za nyakati, tarehe 23 Julai 1946 Luigi wa Consolata akajiunga na watawa wa Shirika la Cottolengo, huko akijita katika sala, huduma kwa wagonjwa mahututi, tafakari, usafi na kilimo. Kunako mwaka 1966 akaweka nadhiri za daima, akaendelea kuchapa kazi na kuwa mfano bora wa kuigwa kwa kuwa na amani ya ndani, tabasamu na utulivu. Akawa mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Kunako tarehe 25 Agosti 1977 akafariki dunia na kwenda kupumzika katika usingizi wa amani, akiwa na umri wa miaka 55.

Kardinali Angelo Amato anabainisha kwamba, Mwenyeheri Luigi wa Consolata alibahatika kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika maisha na utume wake; akaonesha ukuu wa Mungu na utakatifu wa maisha ya binadamu katika sala na tafakari ya kina. Alikuwa ni mtawa aliyejaliwa kuwa na imani thabiti, iliyomwilishwa katika huduma kwa maskini na wagonjwa, daima Yesu na Fumbo la Ekaristi Taktifu, vilikuwa ni kiini cha maisha na utume wake. Hapa akajifunza, kupenda, kuabudu na kuhudumia.

Kardinali Amato anasema kwamba, Mwenyeheri Luigi wa Consolata, aliyakita maisha yake katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; akawaonjesha wengine: huruma, upendo na msamaha uliokuwa unabubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Alibahatika kushuhudia ile dhana ya Kristo Msamaria mwema, aliyeendelea kujisadaka kwa wagonjwa na maskini bila ya kujibakiza hata kidogo, akaonesha ile sura ya Yesu Msamaria mwema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.