2015-05-02 16:09:00

Mshikamano wa upendo na udugu na Wakristo nchini Iraq


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisha ya Mashariki tangu tarehe Mosi hadi tarehe 5 Mei 2015 anafanya ziara ya kikazi nchini Iraq, ili kuwasilisha baraka na mshikamano wa udugu na mapendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, wakati huu wanapokabiliana na hali ngumu katika historia ya maisha yao. Akiwa nchini Iraq, Kardinali Sandri anakutana na viongozi wa Kanisa na Serikali pamoja na Mashirika ya misaada yanayoratibiwa na Shirika la misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO pamoja na kukutana na wakimbizi na wahamiaji.

Mei Mosi, 2015, Siku kuu ya Wafanyakazi duniani, Kardinali Sandri ameadhimisha Ibada ya Ekaristi Takatifu, kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo na kwamba, uwepo wa Roho Mtakatifu unawawezesha kufahamu Maandiko Matakatifu na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Katika Liturujia ya Neno la Mungu amegusia ushuhupavu ulioneshwa na Mtakatifu Paulo wakati alipopelekwa mbele ya Mfalme Agrippa, ambaye alionesha ile hamu ya kutaka kusikiliza Neno la Mungu.

Leo hii, Wakristo nchini Iraq wanakabiliwa na mauaji, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini, kiasi cha kuwafanya wengi wao wakimbie ilikutafuta hifadhi ya maisha. Hata katika hali ya wasi wasi, lakini bado Wakristo wanaonesha ule ujasiri wa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, mahali ambapo waamini wanajichotea chakula kinachowaimarisha katika imani na matumaini, tayari kukabiliana na changamoto za maisha.

Ni mwaliko kwa wale wote wanaofanya madhulumu haya kubadilika na kuanza kujikita katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao badala ya mwelekeo wa sasa wa kuendelea kuharibu kila kitu wanachokutana nacho mbele yao. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inatekeleza dhamana na wajibu wake. Hakuna sababu ya kulipizana kisasi; kwani madhulumu yote haya ni alama ya Msalaba wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, chemchemi ya matumaini mapya kwa waja wake.

Iko siku Yesu Kristo mwenyewe ataweza kupangusa machozi yanayoendelea kububujika kutokana a mateso makali haya. Hakuna sababu ya kukata tamaa, bali kuendelea kuwa na imani na matumaini, ingawa kwa mtu aliyejeruhiwa inakuwa ni vigumu, lakini neema na faraja ya Mungu inapatikana katika sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.