2015-05-02 15:55:00

Marehemu Kard. Giovanni Canestri apumzishwa kwenye usingizi wa amani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi asubuhi, ameshiriki katika Ibada ya Mazishi ya Kardinali Giovanni Canestri, aliyefariki dunia, hivi karibuni, akiwa na umri wa miaka 96. Ni kiongozi wa Kanisa aliyejisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Kama ilivyokuwa kwa Mzee Simeoni, Marehemu Kardinali Canestri angeweza kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa kusema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema, kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu. Ibada ya Misa takatifu imeongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ambaye ametoa pia mahubiri.

Hivi ndiyo mshumaa wa maisha ya Kardinali Canestri ulivyozimika baada ya kutekeleza utume wake Alesandria, Roma, Tortona, Cagliari, Genova na hatimaye, Roma. Kardinali Canestri aliipenda na kuithamini Jumuiya ya Wakristo wa Roma, ambako alitekeleza utume wake kama Padre tangu mwaka 1941 hadi mwaka 1961, akaonesha umahiri wa maisha na wito wa kipadre, hata leo hii bado anakumbukwa katika matukio mbali mbali yaliyojitokeza kwa wakati huo.

Kunako mwaka 1961 Mtakatifu Yohane XXIII akamteua kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma, hapo akafungua ukurasa mpya wa maisha na wito wake kama Kasisi, dhamana ambayo ameitekeleza kwa muda wa miaka 54 kama Askofu. Alishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, akafafanua kwa kina na mapana dhamana na majukumu ya Askofu.

Neno la Mungu anasema Kardinali Sodano linatoa faraja kwa waamini wanaokufa wakiwa na tumaini kwa Kristo na kwamba, wale wanaomwamini watakuwa na maisha tele na Yesu mwenyewe atawafufua siku ya mwisho. Ibada ya Misa takatifu anasema Kardinali Sodano inapania kumweka Marehemu Kardinali Giovanni Canestri mikononi mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma. Kanisa liaadhimisha Ibada hii, likiwa na imani na matumaini katika Fumbo la Kifo na Ufufuko kutoka katika wafu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.