2015-05-01 11:50:00

Uchaguzi mkuu Ethiopia 2015: Jitokezeni kushiriki katika mchakato huu


Pasipo mashauri taifa huanguka, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu. Hii ndiyo kauli mbiu ya ujumbe wa Baraza la Maaskofu katoliki Ethiopia kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Mei 2015. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi, lengo la Kanisa ni kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu kwa binadamu wote.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wake wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo wanakazia umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu na kwa uhuru Zaidi katika kutengeneza sharia, kuongoza dola, kuaminisha kazi na majukumu ya watu na taasisi mbali mbali na hatimaye, katika kuwachagua viongozi wanaopewa ridhaa ya kuonesha dira.

Raia wanakumbushwa kwamba, ni haki na wajibu wao kushiriki katika mchakato wa kupiga kura, kwa ajili ya kuhamasisha mafao ya wengi. Kanisa linawasifu na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwaongoza, kuwatumikia na kutekeleza wajibu wao barabara. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Dhamana ya Afrika, anawahimiza waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa, kitamaduni, kisanaa na katika vyombo vya mawasiliano ya jamii, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Maaskofu Katoliki Ethiopia wanawahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu, kabla na baada  na kwamba, ushiriki huu ni kielelezo cha matumaini na ushuhuda wa ujenzi wa jamii bora inayojikita katika haki. Ni njia muafaka ya kuleta mabadiliko serikalini na katika masuala ya kisiasa kwa kuwachagua viongozi watakaopewa ridhaa ya kuongoza wananchi wa Ethiopia katika kipindi cha miaka mitano.

Viongozi watakaochaguliwa wawe ni sauti ya wanyonge, wanaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni raia waongozwa na kanuni maadili, wenye kuonesha mshikamano wa umoja, udugu na mapendo; watu wenye nguvu ya kimaadili. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, wanasiasa wanapaswa kuwa ni vyombo vya kuponya majanga ya dunia; kwa kujikita katika ustawi na mafao ya wengi na kwamba, uongozi ni kielelezo cha huduma kwa Watu wa Mungu.

Wanasiasa ni watu wanaopaswa kuibua mikakati bora ya kiuchumi na kisiasa, itakayoleta maboresho katika uchumi, afya, elimu. Maaskofu wanaitaka Familia ya Mungu nchini Ethiopia kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kukazia: usawa, haki na Amani; utu na heshima ya binadamu. Ni matumaini yao kwamba, uchaguzi mkuu nchini Ethiopia utakuwa uhuru na wa haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA








All the contents on this site are copyrighted ©.