2015-05-01 07:54:00

Mwenyeheri Junipero Serra: Mtume wa Califonia, kutangazwa Mtakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Marekani, hapo tarehe 23 Septemba 2015, majira ya jioni kwa saa za Marekani, anatarajiwa kumtangaza Fra Junipero Serra, Mtume wa Califonia kama alivyokuwa anajulikana na wengi kuwa Mtakatifu. Hayo yamesemwa na Padre Federico Lombardi, hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa Fra Serra, kama sehemu ya maandalizi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Chuo Kikuu cha Wamarekani, kilichoko hapa mjini Roma, Jumamosi, tarehe 2 Mei 2015.

Baba Mtakatifu Francisko, majira ya saa 6:15 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Chuo kikuu cha Kipapa cha Wamarekani mjini Roma. Hii itakuwa ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kufahamu walau kwa undani zaidi: maisha, utume na mchango wa Fra Junipero Serra. Hili ni tukio ambalo limeandaliwa na Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini kwa kushirikiana na Jimbo kuu la Los Angeles, Marekani.

Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, anasema, Baba Mtakatifu anataka kuwachangamotisha waamini kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mguso, kielelezo cha imani tendaji.

Jumamosi, tarehe 2 Mei 2015, viongozi mbali mbali wa Kanisa watashiriki katika kongamano la siku moja, ili kufafanua kwa kina na mapana: maisha na utume wa Fra Junipero Serra, Mtume wa Califonia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka katika hija yake ya kitume nchini Sri Lanka na Ufilippini, hapo tarehe 15 Januari 2015 aligusia kuhusu Mtawa huyu kutoka katika Shirika la Wafranciskani. Fra Serra alizaliwa kunako mwaka 1713 kwenye Kisiwa cha Maiorca na kufariki dunia kunako mwaka 1784. Akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Yohane Paulo II kunako mwaka 1988.

Ni Mtawa ambaye alijipambanua kwa ari na moyo wa kimissionari, huko Mexico na Califonia ambako alianzisha kazi mbali mbali ambazo hadi leo hii bado zinaendelea kuchanua. Ni mtawa ambaye alisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya wananchi wazawa. Junipero Serra anakuwa ni Mtakatifu wa kwanza Mhispania aliyeishi nchini Marekani kutangazwa kuwa Mtakatifu.

Kumbe, anatarajiwa kuwa ni Mtakatifu na msimamizi wa Wahispania Wakatoliki wanaoishi nchini Marekani, changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa dhati. Hii ni fursa ya kuvunjilia mbali kinzani na utengano kwa misingi ya ukabila na mahali anapotoka mtu.

Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Chuo kikuu cha Kipapa cha Wamarekani, ambacho kinatoa hifadhi kwa Majandokasisi 250 kutoka Marekani. Kwa mara ya kwanza tangu kunako mwaka 1960, Chuo hiki limefurika tena na wanafunzi kutoka Marekani na kwamba, kuna idadikubwa ya wanafunzi ambao wako kwenye orodha ya kusubiri ili kuangalia uwezekano wa kupata nafasi ya kuishi Chuoni hapo na kuendelea na masomo yao hapa mjini Roma. Majandokasisi kutoka Marekani wanajipambanua na wanafunzi wengine kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, mjini Roma na kwenye viunga vyake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.