2015-04-30 07:26:00

Siku kuu ya Wafanyakazi: Lindeni na kutunza haki msingi za wafanyakazi


Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay linasema kwamba, maadhimisho ya Siku kuu ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi, iwe ni siku ya kuhamasisha wadau mbali mbali katika sekta mbali mbali za maisha, kuhakikisha kwamba, wanalinda, wanadumisha na kutetea haki za wafanyakazi. Maaskofu wanapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wafanyakazi wote wanaoendelea kujisadaka katika  kazi mbalimbali mijini na vijijini; watu ambao wanatokwa jasho ili kupata mahitaji yao msingi.

Ni kwa njia ya kazi, watu wanaweza kudumisha utu na heshima yao; tayari kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa njia ya kazi mwanadamu anaendelea kushiriki katika mpango wa Mungu wa kuitengeza dunia ili kweli iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Maaskofu wanapongeza juhudi mbali mbali zinazofanywa kitaifa, ili kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi unatumiwa barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, lakini kwa kutoa kipaumbele kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maaskofu wanapenda kuonesha mshikamano wao wa upendo kwa watu wote wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki; watu wanaosumbuka kutokana na machungu mbali mbali yanayotokana na ukosefu wa fursa za ajira; wafanyakazi waliopata ajali wakiwa kazini au watu ambao wamewapoteza ndugu zao wakiwa kazini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay linakumbusha kwamba, Jumapili ni siku ya: Mungu, Kristo, Kanisa, Binadamu na tafakari ya mambo ya nyakati. Ni siku ya Bwana, ambayo wafanyakazi wanapaswa kujipumzisha ili kuchota nguvu za kiroho na kimwili tayari kupambana na changamoto za maisha. Ni wakati muafaka wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kijamii pamoja na matendo ya huruma.

Jumapili au Domenika ya Bwana ni wakati uliokubalika wa kuungana na waamini wengine kumshukuru, kumtukuza na kumwomba Mwenyezi Mungu, kwa kushiriki katika Chakula cha Neno na Ekaristi, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine. Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay linawaweka wafanyakazi wote chini ya usimamizi na ulinzi wa Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.