2015-04-30 09:05:00

Misale ya Misa kwa Lugha ya Kiswahili, iko mbioni kutolewa!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wa Liturujia waliamua kwa namna ya pekee kukuza na kudumisha maisha ya Kikristo kati ya waamini, kulinganisha taratibu zinazokubalika na mahitaji ya nyakati; kuendelea kuhimiza na kuimarisha mambo yanayosaidia kuleta na kujenga umoja kati ya Wakristo. Lengo kuu ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Ikumbukwe kwamba, Liturujia ni kilele na chemchemi ya maisha ya Kanisa.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliona haja ya kufanya marekebisho katika Liturujia ya Kanisa kwa kuweka vigezo na kanuni za jumla ambazo zinapaswa kufuatwa. Wakigusia kuhusu marekebisho ya vitabu vya Liturujia wanasema, vitabu hivi virekebishwe upesi iwezekanavyo; kazi hii ifanywe na watu wenye ujuzi, na maoni ya Maaskofu wa nchi mbali mbali yasikilizwe. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Umoja.

Kwa kutambua umuhimu wa mabadiliko yaliyofanywa kwenye vitabu vya Liturujia hivi karibuni, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wakati wa maadhimisho ya mkutano wake wa 18 uliofanyika nchini Malawi, kwa pamoja waliamua kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kenya na Tanzania kushirikiana kwa pamoja ili kuandaa Misale ya Altare kwa lugha ya Kiswahili, itakayotumiwa na wazungumzaji wa Kiswahili ndani na nje ya Nchi za AMECEA.

Askofu Salutaris Libena, Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara, anabainisha kwamba, Misale ya Altare kwa lugha ya Kiswahili inatarajiwa kutolewa kabla ya mwisho wa Mwaka 2015. Hii ni kazi iliyofanywa na Kikosi kazi cha Watu 10 kutoka Kenya na Tanzania na kufanya tathmini yao ya pamoja hivi karibuni, Kurasini, Jijini Dar Es Salaam. Itakumbukwa kwamba, tafsiri hii ni ile inayotolewa kutoka katika Lugha ya Kilatini. Hii ni kazi pevu na wala si lele mama inayohitaji tafakari ya kina, umakini na usahihi na tafsiri ya lugha inayotumika.

Askofu Libena anasema, tafsiri ya Misale kadiri ya Kalenda ya Liturujia imekamilika na sasa wanarekebisha baadhi ya sehemuĀ  za Misale hii. Misale pamoja na masomo ya Ibada ya Misa Takatifu itakuwa tayari baada ya kukamilika kwa Misale ya Altare. Muswada wa Misale hii utakapokamilika, utapelekwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kenya na Tanzania kwa mapitio na marekebisho kabla ya kupelekwa Vatican, kwenye Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa, ili kupitishwa na hatimaye, kuchapishwa tayari kwa matumizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.