2015-04-29 15:02:00

Tanzania na Brazil kuendeleza ushirikiano kwa mafao ya nchi hizi mbili


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amekutana na Balozi wa Brazili nchini Tanzania, Bw. Fransisco Luz na kujadiliana mambo kadhaa kuhusu maendeleo na mahusiano baina ya nchi hizo mbili. Akizungumza na Balozi Luz ofisini Magogoni jijini Dar es Salaam Jumatano, Aprili 29, 2015, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi huyo kwa ushirikiano ambao ameutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kipindi cha miaka sita ambacho amekuwa akiiwakilisha nchi yake hapa nchini.

Balozi Luz ambaye amepangiwa kwenda Yordan kwenye kituo kipya, alisema anaondoka nchini akiamini kwamba mtu atakayekuja kumpokea ataendelea mambo aliyoyaanzisha ikiwemo mradi wa kufadhili utafiti na uendelezaji wa zao la pamba kwenye kituo cha utafiti wa kilimo cha Ukiriguru, Mwanza.

Balozi Luz ambaye alifika kumuaga Waziri Mkuu, alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu kwamba ubalozi huo umefanikiwa kupeleka Watanzania wawili kusomea kozi za Uzamili (Masters’ Programme) kwenye vyuo vikuu vya Brazil.“Wanafunzi hawa wawili waliondoka Februari mwaka huu, ni kati ya wanafunzi saba waliofuzu lakini wengine watano walikosa ufadhili kutoka kwenye taasisi zao. Mmoja anasomea Geo-Physics na mwingine Oil Engineering,” alisema Balozi Luz. Balozi Luz ambaye anatarajia kuondoka nchini mapema mwezi ujao, amepangiwa kituo kingine ambapo ataenda kuiwakilisha nchi yake nchini Yordan.

Na Ofisi ya Waziri mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.