2015-04-29 09:41:00

Nani anayetaka kuchochea vita vya kikabila nchini Burundi?


Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanabainisha kwamba, hali ya kisiasa nchini Burundi ni tete na kwamba, wananchi wanaoandamana kupinga Rais Pierre Nkurunziza kuwania madaraka kwa awamu ya tatu tena wanapambana na mkono wa Polisi wa kutuliza ghasia. Wananchi wengi wanasema, kitendo cha Rais Nkurunziza kuwania tena madaraka ni kuvunja Katiba ya nchi. Burundi inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge, Juni 2015, lakini hadi sasa hali si shwari sana na wapenda amani wanahofia kwamba, pengine yakatokea machafuko ya kisiasa na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Taarifa kutoka Bujumbura, zinabainisha kwamba, Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na waandamanaji wanaotaka kuingia mjini. Ofisi na shule zimefungwa mjini Bujumbura kwa hofu ya usalama wa raia na mali zao. Kambi za kijeshi na Seminari kuu ndizo ambazo zinaendelea kufanya shughuli zake za kawaida. Mapambano na ushindani mkubwa unaojitokeza kwa sasa unajikita katika masuala ya kikabila pamoja na uchu wa madaraka, hali ambayo inaweza kusababisha umwagaji wa damu.

Vyama vya kisiasa nchini Burundi vinakanusha madai haya, lakini huu ndio ukweli wa mambo. Jeshi la kukodiwa kutoka DRC na Rwanda liko njiani kuelekea Burundi, taarifa ambayo imekanushwa na Jeshi la Polisi nchini Burundi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.